Michezo Bongo

Samatta Bado Anahitajika, Karia Aweka Wazi Hatua Inayofuata

Vardo July 9, 2026 1:29 pm

RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia, amesema watazungumza na mshambuliaji Mbwana Samatta kuhusu uamuzi wake wa kuacha kuitumikia timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars.

Kauli ya Karia imekuja baada ya Samatta kutangaza kusitisha safari yake ya kuichezea Stars, wakati Tanzania ikiwa inajiandaa kuwa mwenyeji wa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2027.

Karia amesema ameshtushwa na uamuzi huo, ameeleza kuwa si mara ya kwanza kwa Samatta kuonyesha nia ya kuondoka kwenye timu ya taifa, lakini awali walizungumza naye na kumuomba aendelee kwa kuwa bado wanahitaji huduma yake.

“Nimeshtushwa na Samatta, si mara ya kwanza. Aliwahi kuomba na kuandika barua, niliikataa na kuzungumza naye kabla ya AFCON ya Morocco kwa sababu bado tunamhitaji,” amesema Karia.

Amongeza kuwa Samatta amekuwa na mchango mkubwa kwa Stars, akitaja pia nafasi yake ya kupewa unahodha baada ya aliyekuwa nahodha wa muda mrefu, Nadir Haroub ‘Canavaro’.

Karia amesema bado wanaamini Samatta hajafunga kabisa mlango wa kuitumikia Tanzania, hivyo watafanya mazungumzo naye ili kusikiliza sababu zake na kuona kama anaweza kubadili uamuzi wake.

“Samatta bado anacheza, hajastaafu. Tutaongea naye, huwezi kujua ana sababu zake za msingi na tutazisikiliza. Bado hatutaacha kumrai ikiwezekana aweze kuendelea kuitumikia taifa,” amesema Karia.

Yanga Waanze Kujipanga, Beki Simba Aeleza Nguvu Mpya Msimu Ujao Panga La Yanga Laanza Kutema Wachezaji, Wanne Waelekea Singida