Yanga SC

Panga La Yanga Laanza Kutema Wachezaji, Wanne Waelekea Singida

Vardo July 9, 2026 1:33 pm

UONGOZI wa Yanga umeanza kufanya maboresho ya kikosi kuelekea msimu wa 2026/27 baada ya kufanya tathmini ya wachezaji na kuamua kufanya mabadiliko katika baadhi ya maeneo ya timu hiyo.

Taarifa zinaeleza kuwa klabu hiyo imeamua kuachana na baadhi ya nyota ambao hawakuwa sehemu kubwa ya mipango ya kocha, huku wengine wakitarajiwa kutolewa kwa mkopo ili kupata nafasi ya kucheza zaidi.

Miongoni mwa wachezaji wanaotajwa kuondoka Yanga ni Mohammed Damaro na Assink
Frank ambao walikuwa wakicheza kwa mkopo wakitokea Singida Black Stars. Baada ya kumalizika kwa mikataba yao ya mkopo, wawili hao wanatarajiwa kurejea katika klabu yao ya awali.

Mbali na Damaro na Assink, Emmanuel Mwanengo na Israel Mwenda nao wanatajwa kuwa katika wakati mgumu kusalia ndani ya kikosi cha Yanga, huku uwezekano wa kurejeshwa Singida Black Stars ukiendelea kutajwa.

Chanzo cha habari kilieleza kuwa tathmini iliyofanywa na uongozi wa Yanga imebaini umuhimu wa kufanya mabadiliko ili kukipa nguvu zaidi kikosi hicho kuelekea msimu mpya.

“Uongozi umefanya tathmini ya msimu uliopita na kufanya mabadiliko makubwa ndani ya kikosi. Baadhi ya wachezaji wataachwa na wengine kupelekwa kwa mkopo,” kilisema chanzo hicho.

Kwa upande wa Israel Mwenda ambaye bado ana mkataba na Yanga, taarifa zinaeleza kuwa anaweza kutolewa kwa mkopo ili kupata muda zaidi wa kucheza, huku Singida Black Stars ikitajwa kuwa moja ya maeneo yanayoweza kuwa chaguo lake.

Hatua hiyo ni sehemu ya mipango ya Yanga ya kusuka upya kikosi chake baada ya msimu uliopita na kujiandaa kwa changamoto za msimu wa 2026/27.

Samatta Bado Anahitajika, Karia Aweka Wazi  Hatua Inayofuata England Yahaha Kumzuia Erling Haaland