TRA United Yamzidi Yanga Kumsainisha Nasri Kombo
UONGOZI wa TRA United umefanikiwa kufanya usajili mkubwa baada ya kumshawishi nahodha wao, Nasri Kombo, kusalia katika kikosi hicho kwa kuongeza mkataba mpya wa miaka miwili, hatua iliyowapa ushindi mbele ya mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, waliokuwa wakimuwania.
Kombo alikuwa kwenye rada za Yanga kwa muda, huku mabingwa hao wakitajwa kuwa walikuwa tayari kuwasilisha ofa yao kwa ajili ya kumsajili kiungo huyo mwenye uwezo mkubwa.
Hata hivyo, jitihada za TRA United zilifanikiwa baada ya kuweka mezani ofa iliyomvutia mchezaji huyo na kumshawishi kuendelea kuitumikia klabu hiyo.
Taarifa zinaeleza kuwa TRA United ilifanya mazungumzo ya kina na Kombo pamoja na wawakilishi wake, huku uongozi ukisisitiza umuhimu wa nyota huyo kubaki kama sehemu ya mipango yao ya msimu ujao.
Chanzo cha habari kilieleza kuwa Kombo ni miongoni mwa wachezaji ambao watakuwa na maslahi mazuri zaidi ndani ya kikosi cha TRA United, jambo ambalo limekuwa sehemu ya sababu iliyomfanya kuachana na mpango wa kujiunga na Yanga.
“Ni kweli Kombo alikuwa akitakiwa na Yanga ambao walikuwa wameweka ofa yao mezani, lakini mchezaji huyo ameamua kubaki TRA baada ya kupewa ofa nzuri,” kilisema chanzo hicho.
Hatua hiyo imeonekana kuwa ushindi mkubwa kwa TRA United katika kuhakikisha wanabaki na nguzo muhimu ya kikosi chao, huku Yanga wakilazimika kuendelea kutafuta chaguo jingine katika mipango yao ya kuimarisha timu kuelekea msimu wa 2026/27.