Yanga SC

Usajili Mzito Yanga! Flomo Asubiri Baraka Za Al Hilal

Vardo July 14, 2026 7:14 pm

MABINGWA wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, wamekaribia kutikisa tena dirisha la usajili baada ya kufikia makubaliano binafsi na winga mwenye kasi kutoka Liberia, Emmanuel Flomo, huku hatua iliyobaki ikiwa ni kuafikiana na klabu yake ya Al Hilal Omdurman ya Sudan ili kukamilisha dili hilo.

Taarifa kutoka ndani ya mchakato huo zinaeleza kuwa Yanga tayari imefikia makubaliano na Flomo kuhusu masuala muhimu ya mkataba, ikiwemo mshahara, ada ya usajili na muda wa kuitumikia klabu hiyo.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 18 ameridhia kujiunga na mabingwa hao wa Tanzania na kwa sasa anasubiri hatua za mwisho za kukamilisha uhamisho wake.

Baada ya kumaliza mazungumzo na mchezaji, sasa viongozi wa Yanga wameelekeza nguvu zao kwenye mazungumzo na Al Hilal Omdurman, ambayo inamiliki haki za mchezaji huyo. Pande hizo zinatafuta mwafaka utakaowezesha Flomo kuhamia Jangwani kabla ya msimu mpya kuanza.

Flomo ni miongoni mwa vipaji vinavyopewa nafasi kubwa barani Afrika baada ya kuonyesha kiwango bora msimu uliopita. Winga huyo alifunga mabao 12 kwenye ligi na kumaliza katika nafasi ya nne ya wafungaji bora, jambo lililovutia klabu kadhaa kumfuatilia.

Benchi la ufundi la Yanga linaamini ujio wa Flomo utaongeza ushindani na ubora katika safu ya ushambuliaji, huku ukiipa timu nguvu zaidi kuelekea msimu wa 2026/27, ambao utakuwa na changamoto za mashindano ya ndani na kimataifa.

Iwapo mazungumzo kati ya Yanga na Al Hilal yatakamilika kwa mafanikio, Flomo atakuwa miongoni mwa usajili mkubwa na wenye gumzo zaidi ambao Yanga itakuwa imeufanya katika dirisha hili la usajili.

Yanga Yapata Nafuu, FIFA Yaiondolea Adhabu Ya Usajili TRA United Yamzidi Yanga Kumsainisha Nasri Kombo