KVZ Kutua Rwanda: Kocha Hababuu Ali Afichua Mipango Mizito Dhidi ya Rayon Sports Na Ligi ya Mabingwa
KVZ Kutua Rwanda: Kocha Hababuu Ali Afichua Mipango Mizito Dhidi ya Rayon Sports Na Ligi ya Mabingwa
RWANDA: Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Ligi Kuu ya Zanzibar (KVZ), Hababuu Ali, amethibitisha kuwa kikosi chake kimewasili salama nchini Rwanda na kimeshaanaza mazoezi makali kujiandaa na mchezo wao wa kwanza wa Kombe la Kagame dhidi ya Rayon Sports.
KVZ iliondoka Zanzibar Julai 20, 2026, kuelekea Rwanda kushiriki michuano hiyo mikubwa ya ukanda wa CECAFA ikiwa ni mara yao ya kwanza. Vijana hao wa Zanzibar wanatarajiwa kushuka dimbani Jumapili hii kuvaana na wenyej wao, Rayon Sports.
Akizungumzia maandalizi ya timu hiyo, Kocha Hababuu amebainisha kuwa KVZ ina malengo makuu mawili katika michuano hiyo: kupata uzoefu wa kimataifa pamoja na kujiweka sawa kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Tumejipanga vizuri kucheza na Rayon Sports. Wachezaji wamefika salama na wanaendelea na mazoezi kwa morali ya juu. Tunaamini tutafanya vizuri na kupata matokeo chanya katika mchezo huu,” amesema Kocha Hababuu.
Kipimo Sahihi Kabla ya Kimataifa
Mwalimu huyo aliongeza kuwa, ingawa KVZ imepangwa katika Kundi C lenye timu zenye uzoefu na mataji mengi, hiyo si sababu ya wao kukata tamaa au kushindwa kutimiza malengo yao.
“Kwa kipindi hiki kupata mechi za ushindani wa kiwango cha kimataifa si jambo rahisi. Hivyo, tunahakikisha tunaitumia fursa hii kikamilifu kujipima dhidi ya timu zenye ubora mkubwa,” aliongeza.
Benchi la ufundi la KVZ limesisitiza kuwa lengo lao kuu si tu kupata matokeo mazuri kwenye Kombe la Kagame, bali pia kujenga kikosi imara na chenye ushindani kitakachokuwa tayari kwa mchakamchaka wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
🗓️ Ratiba ya KVZ (Kundi C):
-
Julai 26: Rayon Sports (Rwanda) vs KVZ
-
Julai 29: KVZ vs Al Hilal (Sudan)
-
Agosti 1: Tusker (Kenya) vs KVZ