CECAFA Kagame Cup 2026: Simba na Singida Black Stars Kuanza Kazi Leo Kigali
WAWAKILISHI wa Tanzania Bara katika michuano ya CECAFA Kagame Cup 2026, Singida Black Stars na Simba SC, leo Jumamosi (Julai 25, 2026) wanashuka dimbani mjini Kigali, Rwanda, kuanza rasmi vita ya kusaka ubingwa wa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Michuano hiyo iliyoanza Ijumaa ya Julai 24, inatarajiwa kutimua vumbi kwa mechi kali huku timu zote mbili kutoka Tanzania zikiwa na nia moja tu: kuanza na ushindi mnono.
Singida Black Stars Kuanza Kutetea Taji Dhidi ya Jamus FC
Mabingwa watetezi wa michuano hii, Singida Black Stars, wanatarajiwa kufungua ratiba yao kwa kuvaana na Jamus FC kutoka Sudan Kusini. Mechi hiyo itapigwa kuanzia saa 9:00 alasiri katika Uwanja wa Kigali Pele.
Singida wanaingia uwanjani wakiwa na presha na hamu ya kutetea taji walilolitwaa mwaka jana, huku wakitambua ushindi wa mechi ya kwanza utawapa njia rahisi ya kutinga hatua inayofuata.
Simba SC Kuanza Kusaka Taji la 7 Dhidi ya Mogadishu City
Kwa upande wa Simba SC, wao watakuwa na kibarua kizito dhidi ya Mogadishu City kutoka Somalia katika uwanja huo huo wa Kigali Pele kuanzia saa 12:00 jioni.
Wekundu wa Msimbazi wanaingia kwenye mashindano haya wakiwa na rekodi ya kipekee ya kuwa klabu yenye mafanikio makubwa zaidi katika historia ya CECAFA Kagame Cup, ikiwa imetwaa ubingwa mara 6 (1974, 1991, 1992, 1995, 1996, na 2002). Ushindi katika michuano ya mwaka huu utaifanya Simba ifikishe mataji 7 na kuendelea kuandika historia mpya.
Rais wa CECAFA Aipongeza Rwanda na Rais Paul Kagame
Wakati huohuo, Rais wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Paulos Weldehaimanot Andemariam, amesema michuano ya mwaka huu itakuwa bora zaidi kuwahi kutokea kutokana na maandalizi kabambe yaliyofanywa na Rwanda.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Uwanja wa Amahoro, Kigali, Andemariam aliishukuru Serikali ya Rwanda chini ya Rais Paul Kagame pamoja na Shirikisho la Soka Rwanda (FERWAFA):
“Ninaishukuru Serikali ya Rwanda chini ya Rais Paul Kagame na uongozi wa FERWAFA kwa kurudisha mashindano haya Rwanda kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2019. Tuna imani kubwa yatakuwa mashindano bora zaidi ya CECAFA Kagame Cup,” alisema Andemariam.
Zawadi Nonos kwa Washindi wa CECAFA Kagame Cup 2026
Mashindano ya mwaka huu yanashirikisha timu 12 kutoka nchi 9, huku fainali ikitarajiwa kuchezwa Agosti 7, 2026.
Mchanganuo wa Zawadi:
-
🥇 Mbingwa: Dola $30,000 (Zaidi ya TZS Milioni 81)
-
🥈 Mshindi wa Pili: Dola $20,000 (Zaidi ya TZS Milioni 54)
-
🥉 Mshindi wa Tatu: Dola $10,000 (Zaidi ya TZS Milioni 27)
Tangu mwaka 2002, Rais Paul Kagame amekuwa akidhamini fedha za zawadi za mashindano haya, jambo lililosaidia kuongeza thamani na ushindani wa soka katika ukanda wa CECAFA.
Makundi ya CECAFA Kagame Cup 2026
-
Kundi A: APR (Rwanda), Vipers SC (Uganda), Gor Mahia (Kenya), Garde Republicaine (Djibouti)
-
Kundi B: Singida Black Stars (Tanzania), Simba SC (Tanzania), Jamus FC (Sudan Kusini), Mogadishu City (Somalia)
-
Kundi C: Al Hilal (Sudan), Rayon Sports (Rwanda), Tusker FC (Kenya), KVZ (Zanzibar)