Hersi Said Afunguka Mazito Yanga: Usajili Mpya na Sababu za Timu Kushuka Kiwango
Rais wa Klabu ya Yanga, Hersi Said, ameweka wazi hisia zake za ndani kuhusu mwenendo wa timu hiyo msimu uliopita, akikiri kuwa ingawa walifanikiwa kutwaa baadhi ya mataji, kiwango cha uwanjani hakikumpendeza yeye, wachezaji, wala mashabiki.
Akizungumzia maandalizi kuelekea msimu mpya wa 2026/27, Hersi ameeleza kuwa changamoto kubwa iliyochangia kuporomoka kwa ubora wa timu ni pamoja na usajili kutotoa matokeo yaliyotarajiwa pamoja na majeraha ya mara kwa mara yaliyowakumba wachezaji tegemeo.
“Kulikuwa na wakati nilifika hatua sipendi hata kuangalia mechi za timu yangu. Naamini hata ninyi mashabiki mlipitia hisia hizo hizo,” alisema Hersi kwa uchungu.
Mabadiliko Makubwa na Usajili Mpyaw
Ili kukabiliana na changamoto hizo, uongozi wa Yanga umerudi kwenye uwanja wa hesabu na kufanya tathmini ya kina. Hersi amesisitiza kuwa tayari wameanza kufanya usajili wa nguvu ili kuhakikisha makosa ya msimu uliopita hayajirudii tena.
Ameongeza kuwa mashabiki wakae tayari kwani pazia la usajili bado halijafungwa, na lengo kuu ni kurejesha furaha na soka la ushindani linalojulikana na kila mwana-Yanga.
“Tumefanya usajili mkubwa kwa sababu hatutaki kurudia makosa yale. Ilifika wakati tulikuwa tunaomba mechi ziishe haraka, na nadhani hayo si maisha tuliyoizoea Yanga. Bado hatujamaliza kusajili, tunataka kikosi kitakachowapa mashabiki raha waliyoizoea,” alihitimisha Hersi Said.