Jammy Simba Petrojet
Michezo Bongo

Jammy Simba Agusa Petrojet ya Misri: Mkataba wa Miaka 3 Mezani!

Vardo August 6, 2026 11:14 am

Mshambuliaji machachari wa Kitanzania, Jammy Simba, yuko hatua za mwisho kukamilisha uhamisho wake kwenda klabu ya Petrojet FC inayoshiriki Ligi Kuu nchini Misri, kufuatia makubaliano ya awali kati ya pande zote mbili.

Uhamisho huu unakuja kama tuzo kwa nyota huyo baada ya kuonyesha kiwango cha juu na cha kuridhisha akiwa na klabu ya KMC katika msimu wa 2025-2026, licha ya changamoto zilizoikabili timu hiyo na kupelekea kushuka daraja.

Mkataba wa Miaka 3 na Kipengele cha Nyongeza

Taarifa kutoka kwa mtu wa karibu wa mchezaji huyo zinaeleza kuwa mazungumzo yamefikia hatua nzuri na zimebaki maelezo machache tu kabla ya kuweka saini kwenye mkataba wa miaka mitatu (3), wenye kipengele cha kuongeza msimu mmoja zaidi.

“Kila kitu kinaenda vizuri na tunatarajia muda wowote kuanzia sasa tutakamilisha uhamisho huo. Petrojet imevutiwa sana na kipaji chake. Ni hatua kubwa kwake binafsi na kwa soka la Tanzania kwa ujumla,” kilieleza chanzo hicho.

Mbali na Petrojet, klabu nyingine ya nchini Misri, Petrol Asyout, nayo imeonyesha nia ya dhati ya kuwania saini ya mshambuliaji huyo.

Kutoka JKU Hadi Soka la Kimataifa

Simba (20), aliyezaliwa Julai 15, 2006, alijiunga na KMC katika dirisha dogo la usajili la Januari 2025 akitokea klabu ya JKU ya Zanzibar. Ufanisi wake ulimwezesha pia kupata nafasi katika kikosi cha Timu ya Taifa ya Tanzania ya vijana chini ya miaka 20 (U-20).

Kama mpango huu utakamilika, Jammy Simba atakuwa mchezaji wa pili hivi karibuni kutoka KMC kuelekea Misri, akifuata nyayo za beki Rahim Shomary aliyejiunga na Ghazl El Mahalla mnamo Julai 2025.

Kocha Barker Afichua Mpango Mzito Simba SC Baada ya Kurejea Rwanda KVZ Yatwaa Ubingwa wa Ligi ya Netiboli Zanzibar Mara ya 6 Mfululizo!