Ukweli wa Fei Toto Kutakiwa Simba na Yanga Huu Hapa!
Rais wa Azam FC, Nassor Idrissa ‘Father’, hatimaye amevunja ukimya na kuweka mambo hadharani kuhusu tetesi zinazomhusisha kiungo wao machachari, Feisal Salum ‘Fei Toto’, na miamba ya soka nchini, Simba SC na Yanga SC.
Fei Toto amekuwa gumzo kubwa katika dirisha hili la usajili, huku taarifa zikisema klabu hizo kongwe za Tanzania zinachuana vikali kuwania saini yake, kila mmoja akiwa tayari kutoa dau nono ili kumng’oa Azam FC.
Hata hivyo, bosi huyo wa Azam FC ameweka wazi msimamo wa klabu na kuondoa hofu kwa mashabiki wao. Father amethibitisha kuwa Fei Toto bado ni mchezaji halali wa Azam FC na ana mkataba unaomfunga kuendelea kuichezea klabu hiyo kwa misimu ijayo.
Amesisitiza kuwa maneno na uvumi unaoenea mtaani kuhusu usajili huo haubadilishi ukweli wowote, na kwamba kiungo huyo yupo kwenye mipango madhubuti ya timu kuelekea msimu mpya wa mashindano.
“Fei yupo kambini nchini Rwanda na anaendelea na mazoezi makali pamoja na wenzake kujiandaa na msimu mpya wa mashindano,” alisema Father.