Alassane Kante Simba SC
Simba SC

Hatima ya Alassane Kante Simba SC Msimu wa 2026/27 Yafichuka

Vardo August 8, 2026 10:06 pm

Suala la kiungo raia wa Senegal, Alassane Kante, limeendelea kuzua gumzo miongoni mwa mashabiki wa Msimbazi baada ya jina lake kukosekana rasmi katika orodha ya wachezaji watakaotumiwa na klabu ya Simba SC kwa msimu wa 2026/27.

Kante hakuonekana kabisa wakati wa utambulisho wa kikosi cha wachezaji 31 kwenye tamasha la Simba Day, hali iliyoibua maswali mengi kutoka kwa mashabiki waliotaka kufahamu hatima ya nyota huyo.

Kauli ya Ahmed Ally Kuhusu Kante

Akizungumzia utata huo, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, ameweka wazi kuwa mchezaji huyo bado ana mkataba na klabu hiyo na taarifa rasmi kuhusu mustakabali wake zitatolewa hivi karibuni.

“Naomba niseme jambo moja kuhusu Kante; bado ni mchezaji wetu na taarifa zake kamili tutazitoa baadaye,” alisema Ahmed Ally.

Ushindani wa Namba na Idadi ya Wageni

Pamoja na maelezo hayo, taarifa za ndani zinaeleza kuwa Kante amekuwa akiachwa kwenye mipango ya timu hatua kwa hatua. Mpaka sasa, Simba SC imekamilisha utambulisho wa wachezaji 12 wa kigeni, idadi inayojaza nafasi zote za wageni kulingana na kanuni.

Kiungo huyo alijiunga na Simba SC mnamo Julai 23, 2025, akitokea CA Bizertin ya Tunisia baada ya kuonyesha kiwango cha juu. Hata hivyo, ushindani mkubwa wa namba kikosini na ongezeko la nyota wapya wa kigeni umeonekana kuweka finyu fursa yake ya kusalia Msimbazi.

Kwa sasa, macho na masikio ya wana-Simba yanalenga uongozi wa klabu hiyo kusubiri taarifa ya mwisho kuhusu sehemu atakayoelekea Kante kabla ya dirisha la usajili kufungwa rasmi.

Mo Dewji Wazi: Aweka Mezani Bilioni 30 Kuisuka Simba Upya