Mo Dewji Aweka Wazi Mipango Mizito Simba SC Miaka 90: “Tutateka Afrika”
RAIS wa Simba, Mohammed Dewji ‘Mo’, amesema anaamini klabu hiyo inaweza kufanya makubwa zaidi katika soka la Afrika katika miaka ijayo kuliko ilivyowahi kufanya katika historia yake ya miaka 90.
Kauli hiyo imekuja wakati Simba ikitimiza miaka 90 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1936, huku leo ikitarajiwa kuadhimisha tukio hilo kupitia tamasha la Simba Day litakalofanyika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Katika kilele cha tamasha hilo, Simba itacheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Police FC ya Kenya, huku tukio hilo likitumika pia kuwa sehemu ya maandalizi ya kikosi hicho kuelekea msimu mpya wa 2026/27.
Mo amesema kila kipindi amekuwa akishuhudia mabadiliko ndani ya Simba, jambo linalompa matumaini makubwa kwamba klabu hiyo inaweza kufikia hatua kubwa zaidi barani Afrika.
“Ninaamini kwa kipindi kijacho timu hii inaweza kufanya mambo makubwa zaidi Afrika kuliko ilivyofanya katika miaka 90 iliyopita,” amesema Mo.
Amesema mafanikio ya Simba hayajaja kwa bahati, bali yamejengwa na mchango wa watu mbalimbali waliowahi kuwa sehemu ya klabu hiyo, akiwamo wachezaji, makocha na viongozi.
Kuhusu mchezaji bora katika historia ya Simba, Mo amesema klabu hiyo imewahi kuwa na wachezaji wengi wenye uwezo mkubwa, hivyo si rahisi kumtaja mmoja pekee.
Mo, ambaye kabla ya kuwa mwekezaji alikuwa shabiki kindakindaki wa Simba, amesema baadhi ya wachezaji waliowahi kuichezea klabu hiyo wameacha alama kubwa na kwa mtazamo wake wanastahili kukumbukwa katika historia ya Simba.
Amesema anaheshimu mchango wa kila mmoja aliyewahi kuitumikia Simba, akisisitiza kuwa mafanikio ya klabu hiyo yamejengwa na vizazi mbalimbali vilivyopitia katika klabu hiyo.
Chini ya uongozi wa Mo, Simba imeendelea kujijenga kama moja ya klabu kubwa na zenye ushawishi Tanzania na Afrika, huku matarajio yake sasa yakiwa ni kuona klabu hiyo ikipiga hatua zaidi katika mashindano ya kimataifa.
Kwa Simba, maadhimisho ya miaka 90 si kumbukumbu ya historia pekee, bali pia ni mwanzo wa safari mpya yenye lengo la kuifanya klabu hiyo kuandika ukurasa mwingine mkubwa katika soka la Afrika.