CECAFA Women’s: Simba Queens Yaanza na Ushindi Mnono Rwanda, Yainyuka Top Girls 2-0!
Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania, Simba Queens, wameanza vyema kampeni yao ya kusaka ubingwa wa CECAFA Women’s Champions League baada ya kuibuka na ushindi mnono wa mabao 2-0 dhidi ya Top Girls Academy ya Burundi, katika mchezo uliochezwa nchini Rwanda.
Kikosi hicho cha Simba Queens kilionyesha kiwango cha juu na kutawala mchezo muda wote, huku wakitumia vyema nafasi walizotengeneza kupata ushindi huo muhimu katika hatua ya makundi ya michuano hiyo ya ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Wafungaji wa Mabao ya Simba Queens Nyota wa kikosi hicho, Aisha Mnuka, ndiye aliyefungua ukurasa wa mabao kwa shuti kali na kuifanya Simba Queens kuongoza, kabla ya Kusamfulaa Rida kupiga msumari wa pili na kukamilisha ushindi huo wa mabao 2-0.
Lengo Kuu la Simba Queens CECAFA Ushindi huu unawapa Simba Queens mwanzo mzuri na hamasa kubwa katika safari yao ya kuwakilisha nchi. Lengo kuu la timu hiyo nchini Rwanda ni kutwaa ubingwa wa CECAFA Women’s Champions League, kwani timu itakayotwaa ndoo hiyo ndiyo itakayopata tiketi ya moja kwa moja kuiwakilisha kanda hiyo kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake (CAF Women’s Champions League).
Kwa matokeo haya ya kwanza, Simba Queens imeonyesha nia ya dhati ya kuandika historia nyingine na kuendelea kuipa Tanzania heshima kubwa katika jukwaa la soka la kimataifa.