Simba Yainyuka Singida Black Stars 2-1 Ligi Kuu: Ubabe wa Pungufu Ukiendelea!
Licha ya kulazimika kucheza pungufu kwa mchezo mwingine mfululizo, Simba SC imeendelea kuonyesha umwamba wake katika Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Singida Black Stars kwenye Uwanja wa Airtel, Singida.
Wekundu wa Msimbazi waliaza mchezo huo kwa kasi ya ajabu na kupata bao la kuongoza mapema katika dakika ya 12 kupitia kwa kiungo wao, Clatous Chama. Chama alimalizia kwa umakini mpira wa pasi kutoka kwa Libasse Gueye, kufuatia kazi nzuri na krosi iliyochongwa na Elie Mpanzu.
Wenyeji Singida Black Stars walijibu mapigo katika dakika ya 22 baada ya Shekhan Ibrahim kufunga bao la kusawazisha na kufanya matokeo kuwa 1-1, matokeo yaliyodumu mpaka timu zote mbili zilipoenda mapumziko.
Kipindi cha pili kilianza kwa Simba kuongeza presha na juhudi zao zililipa katika dakika ya 63 pale walipojipatia mkwaju wa penalti. Beki Rushein De Reuck alisimama vyema na kupiga penalti hiyo iliyomwacha kipa wa Singida bila fursa, na kuiweka Simba mbele kwa mabao 2-1.
Baada ya bao hilo, Simba ilipambana kwa nidhamu ya hali ya juu kulinda ushindi huo mpaka dakika 90 zinakamilika na kuondoka na pointi zote tatu muhimu ugenini.
Ushindi huu unaifanya Simba kufikisha pointi 9 kamili baada ya kushinda michezo yake yote mitatu ya kwanza msimu huu, ikianza na Kagera Sugar, ikafuata Pamba Jiji na sasa Singida Black Stars. Kinachoshangaza na kuwavutia wengi ni jinsi Simba ilivyoweza kushinda mechi zote hizi tatu ikiwa na wachezaji pungufu uwanjani baada ya kadi nyekundu, lakini bado ikaendelea kukusanya pointi kwa kishindo na kukaa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu.