Rekodi Mbaya! Simba Yafikisha Kadi Nyekundu Tatu Ligi Kuu 2026/27
Klabu ya Simba SC imeanza msimu wa 2026/27 wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kuweka rekodi isiyovutia, baada ya wachezaji wake kuonyeshwa kadi nyekundu katika kila mchezo wa ligi waliocheza hadi sasa.
Mfululizo huo wa kadi umeidhinishwa leo baada ya beki Antony Mligo kuonyeshwa kadi nyekundu katika mchezo dhidi ya Singida Black Stars, uliopigwa kwenye Uwanja wa Liti, Singida. Adhabu hiyo imeifanya Simba kufikisha kadi nyekundu tatu katika michezo mitatu mfululizo, hali inayozua mjadala mkubwa miongoni mwa mashabiki wa soka nchini.
Mwenendo huu ulianza katika mchezo wa kwanza wa msimu dhidi ya Kagera Sugar, ambapo Simba walimkosa beki wao David Kameta ‘Duchu’ kwa kadi nyekundu. Kabla ya mshtuko wa tukio hilo kutulia, mchezo uliofuata dhidi ya Pamba Jiji ulishuhudia kiungo Ibraheem Jabaar akitolewa pia kwa kadi nyekundu.
Hali hii inamweka kocha mkuu Steve Barker katika wakati mgumu wa kusuka safu yake ya ulinzi na nidhamu ya timu kwa ujumla. Barker ana kazi kubwa ya kuhakikisha anadhibiti nidhamu ya wachezaji uwanjani ili kuepuka kupoteza nguvu kazi muhimu mapema kwenye msimu wenye ratiba ndefu na yenye ushindani mkali.
Japo Simba ilianza msimu kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Kagera Sugar kabla ya kucheza na Pamba Jiji na Singida Black Stars, suala la kadi nyekundu limekuwa doa katika mwanzo wao wa msimu. Macho ya mashabiki sasa yameelekezwa kwenye mchezo wao unaofuata kuona kama timu hiyo itaweza kumaliza mchezo ikiwa na wachezaji wote 11 uwanjani.