Ibenge Awashusha Presha Mashabiki wa Azam FC: “Tunasubiri Mechi 7 Tu!”
Kocha Mkuu wa Azam FC, Florent Ibenge, amewataka mashabiki wa klabu hiyo kuwa na subira na kuondoa wasiwasi juu ya kiwango cha timu hiyo kwenye mwanzo wa msimu wa Ligi Kuu Bara. Ibenge amebainisha kuwa kikosi chake kinahitaji angalau mechi saba ili kucheza kwa kiwango bora kinachotarajiwa.
Azam FC ilianza msimu kwa matokeo ya kusuasua baada ya kutoka sare ya 1-1 ugenini dhidi ya Polisi Tanzania, kabla ya kuibuka na ushindi mgumu wa mabao 2-1 nyumbani dhidi ya TRA United—mchezo ambao kipa wao Aishi Manula alionyeshwa kadi nyekundu.
Sababu ya Kiwango Kusuasua na Muunganiko wa Timu
Akizungumza kuhusu muonekano wa timu yake, Ibenge ameeleza kuwa kutokana na muda mfupi wa maandalizi kabla ya msimu kuanza (pre-season), timu bado inatafuta muunganiko sahihi kati ya wachezaji wapya na wale waliosalia.
“Hatukupata muda wa kutosha kwenye maandalizi yetu ya mwanzo wa msimu, lakini hatulalamiki. Kitu tunachotakiwa kukifanya haraka ni kutafuta muunganiko wa wachezaji tuliowaongeza na wale waliobaki. Kuna wachezaji wapya wameanza kuzoea haraka, na waliobaki ndio uti wa mgongo wa timu,” alisema Ibenge.
Mechi Saba Kuthibisha Ubora Wa Azam FC
Kocha huyo raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amesisitiza kuwa ushindi uliopita dhidi ya TRA United ulikuwa muhimu kwa ajili ya kujenga kujiamini kwa wachezaji, na sasa wanahitaji mechi chache zaidi ili kukaa sawa.
“Nafahamu mashabiki wanahitaji Azam iliyo bora. Tuna timu nzuri lakini tunahitaji kama mechi saba hivi ili kucheza kwa ubora tunaotamani. Jambo zuri ni kwamba tumerudi kwenye njia ya ushindi.”
Baada ya ushindi huo, Azam FC ilishuka dimbani kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi kuwakabili Pamba Jiji kutoka Mwanza katika mechi yao ya tatu ya Ligi Kuu Bara.