Kigogo wa Yanga Atoa Onyo Zito: “Kuna Timu Utakuja Kufungwa Mabao 10 Msimu Huu”
Kiwango cha kuvutia ambacho kikosi cha Young Africans (Yanga SC) kimeanza kukionyesha msimu huu hakiwafurahishi mashabiki pekee, bali kinawapa furaha kubwa viongozi wa klabu hiyo, huku mmoja wa viongozi wa juu akituma onyo kali kwa wapinzani.
Katika dirisha la usajili lililopita, Yanga ilifanya maboresho makubwa kwa kusajili jumla ya wachezaji 14 vipaji vya kimataifa na nyota wa hapa nyumbani ili kuimarisha maeneo yote ya uwanja.
Akizungumza kuhusu mwenendo wa timu hiyo, Makamu wa Rais wa Yanga, Arafat Haji, alieleza kuwa usajili uliofanywa umeanza kuzaa matunda mapema na kutoa picha halisi ya msimu utakavyokuwa.
“Nipongeze uongozi kwa ujumla, hasa kwenye hesabu za usajili. Kuna kazi kubwa imefanyika ya kusajili wachezaji ambao wanatoa mchango mkubwa ndani ya kikosi pamoja na benchi la ufundi,” alisema Arafat.
Arafat aliongeza kuwa benchi la ufundi limefanya kazi kubwa ya kuunganisha wachezaji wapya na wa zamani, jambo linalowapa nguvu viongozi kutokana na malengo waliyojiwekea kuanza kutimia.
“Msimu huu kuna uwezekano mkubwa wa timu yetu kucheza kwa ubora zaidi na kuwa tishio kubwa. Naamini kuna timu inaweza kufungwa hata mabao 10 kutokana na idadi kubwa ya nafasi zinazotengenezwa na kutumiwa vizuri,” aliongeza.
Mpaka sasa, Yanga SC haijapoteza mchezo wowote katika mechi zake tatu za kwanza za Ligi Kuu Bara. Timu hiyo imeshinda mechi zote ikifunga jumla ya mabao 11 na kuruhusu mabao mawili pekee—ikiifunga Namungo FC (3-1), Coastal Union (4-1), na JKT Tanzania (4-0).
Nyota wapya walioanza kuonyesha cheche zao ni pamoja na Albert Kangwanda (mabao 2 na asisti 1), Peter Shalulile (mabao 2), na Housseine Zakouani ambaye tayari ametengeneza asisti tatu.