Hamisa Mobetto na Aziz KI
Burudani

Hamisa Mobetto Afunguka Siri ya Ndoa Yake na Aziz KI, Ubalozi UNESCO na Ng’ombe 30 za Mahari

Vardo August 28, 2026 6:22 pm

Mwanamitindo na mfanyabiashara mashuhuri nchini, Hamisa Mobetto, amefunguka kwa mara ya kwanza kuhusu maisha yake ya ndoa na mumewe, Stephane Aziz KI, huku akibainisha siri iliyomfikisha kwenye mafanikio makubwa ya kupata mikataba minono ya ubalozi.

Akiyasema hayo mara baada ya kutambulishwa rasmi kuwa UNESCO Global Champion—nafasi inayolenga kuhamasisha matumizi salama na yenye tija ya mitandao ya kijamii kwa wanawake na wasichana—Hamisa alieleza kuwa safari yao ya ndoa haikutokea kwa haraka kama watu wengi wanavyofikiria.

Miaka 3 ya Mahusiano ya Siri Akizungumzia mahusiano yake na kiungo mshambuliaji huyo mahiri wa Yanga na timu ya taifa ya Burkina Faso, Hamisa alisema walichukua takribani miaka mitatu kujenga msingi madhubuti wa uhusiano wao kabla ya kufanya maamuzi ya kufunga ndoa.

“Tulikuwa kwenye mahusiano kwa muda wa miaka mitatu kabla ya kuamua kuingia kwenye ndoa. Hatukuharakisha kuweka kila kitu wazi kwenye mitandao ya kijamii, tulisubiri wakati mwafaka. Hii ilitusaidia sana kulinda maisha yetu binafsi,” alieleza Hamisa.

Siri ya Mikataba ya Ubalozi na Mafanikio Kuhusu kuendelea kuaminika na makampuni makubwa pamoja na mashirika ya kimataifa, Hamisa amesema mafanikio hayo hayaji kwa bahati mbaya bali yanahitaji nidhamu ya juu na kazi ngumu.

Alitaja kumtanguliza Mwenyezi Mungu, kuheshimu mikataba, na kuwa mwaminifu kwa bidhaa au makampuni anayofanya nayo kazi kuwa ndio nguzo kuu zinazomfanya aendelee kuaminika siku hadi siku.

Je, Ng’ombe 30 za Mahari Ziko Wapi? Akiulizwa kuhusu hatua iliyofikiwa na ng’ombe 30 wa mahari waliotolewa na Aziz KI wakati wa taratibu za ndoa yao—kama wameongezeka au la—Hamisa alijibu kwa utani kuwa suala hilo lipo mikononi mwa mama yake mzazi.

“Hilo mama yangu ndiye anayelipatia majawabu kwa sababu mimi binafsi sikuchukua hata ng’ombe mmoja, kwani yote hayo yalimhusu yeye,” alisema.

Matumizi Sahihi ya Mitandao ya Kijamii Hamisa alihitimisha kwa kueleza kuwa mitandao ya kijamii imekuwa nguzo muhimu katika kujenga jina lake na kumfungulia fursa za kibiashara na kifamilia. Kupitia nafasi yake mpya UNESCO, amedhamiria kuwatumia vijana na mabinti kutumia fursa za kidijitali kujikwamua kiuchumi badala ya kuitumia mitandao hiyo kwa mambo yanayoweza kuwaletea madhara.

Meridianbet Yaisogeza Fortune Eagle Kukupa Bahati Mashabiki Simba Mbeya Waandaa Coaster 5 Kuivamia Mighty Wanderers Malawi