Simba SC Yafunguka Hali ya Majeruhi: Kagoma, Kibabage na Hatima ya Alassane Kanté
SIMBA imeweka wazi hali ya wachezaji wake majeruhi, huku ikithibitisha kuwa Yusuf Kagoma na Nickson Kibabage ni miongoni mwa wachezaji ambao hawakuweza kuwa sehemu ya kikosi katika mchezo wa jana.
Akizungumza kuhusu hali ya kikosi hicho, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema bado anasubiri ripoti kutoka kwa madaktari ili kupata taarifa kamili kuhusu maendeleo ya majeruhi waliopo kwenye kikosi.
Ahmed amesema wachezaji wengine wamekuwa wakicheza huku wakiwa na majeraha madogo kutokana na hamu yao ya kuipambania timu, akisisitiza kuwa utayari wao wa kucheza haupaswi kuchukuliwa kama kutokuwepo kwa changamoto za kiafya.
“Wachezaji wanaumia na wengine wanacheza na majeruhi, ni vile tu wanataka kuipambania timu yao. Wanapata na kazi ya kucheza,” amesema Ahmed.
Almefafanua kuwa kwa taarifa walizonazo hadi sasa, Kagoma alikosa mchezo huo kutokana na hali yake ya majeraha, wakati Kibabage pia bado anaendelea na matibabu.
“Mpaka sasa status ya majeruhi ambao tuko nao ni Yusuf Kagoma ambaye amekosekana kwenye mchezo leo, pamoja na Nickson Kibabage ambaye naye ni majeruhi,” amesema.
Hata hivyo, Ahmed amessema wachezaji wengine waliopo kwenye kikosi wako katika hali nzuri na wanaendelea na majukumu yao, huku waliokuwa na changamoto za kadi wakitengwa na suala la majeraha.
Katika hatua nyingine, Ahmed alizungumzia pia suala la kiungo Alassane Kanté, ambaye hakutambulishwa katika hafla ya Simba Day, lakini amekuwa akihusishwa na klabu hiyo.
Ahmed alisema Kanté bado ni mchezaji wa Simba mwenye mkataba na klabu hiyo, lakini kuna taratibu za ndani zinazoendelea ambazo bado hazijafikia hatua ya kutolewa hadharani.
“Tulimwita kuwa ni mchezaji wetu, ni mchezaji wa Simba. Bado ana mkataba na ziko taratibu za ndani ambazo zinaendelea. Zikikamilika tutawaambia status ya Alassane Kanté na Simba,” amesema.
Kwa mujibu wa Ahmed, klabu hiyo bado haipo tayari kueleza kwa undani mipango inayohusu Kanté, ikisisitiza kuwa muda wa kufanya hivyo bado haujafika.
“Ni mchezaji wetu na kuna mipango ambayo inaendelea. Haitakuwa sawa kuitaja sasa kwa sababu bado haijafika mwisho,” ameongeza.
Kauli hiyo imeacha wazi kuwa suala la Kanté bado linaendelea kushughulikiwa ndani ya Simba, huku mashabiki wakisubiri kuona hatima yake ndani ya kikosi hicho.