Kocha wa Simba Steve Barker
Simba SC

BARKER AKANYAGA BREKI SIMBA: Azungumzia Safari ya Malawi, Majeruhi Kurejea na Rekodi ya Ushindi 15

Vardo September 1, 2026 5:47 pm

BAADA ya kukimbizana na ratiba ngumu pamoja na kufikisha mfululizo wa ushindi wa mechi 15 kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, Kocha Mkuu wa Simba, Steve Barker, ameamua kuwapa mapumziko mafupi wachezaji wake ili kujiandaa na vita ya kimataifa.

Simba sasa inahamishia nguvu zake zote kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF Champions League), ambapo inatarajiwa kusafiri kuelekea Malawi kukipiga dhidi ya Mighty Wanderers katika mchezo wa hatua ya awali.

Mapumziko Kabla ya Safari ya Malawi

Kocha Barker amebainisha kuwa msongamano wa mechi uliwajaza uchovu wachezaji, hivyo siku moja ya mapumziko ilikuwa lazima kabla ya kuanza maandalizi ya mwisho ya safari.

“Tumekuwa tukicheza mechi nyingi kwa muda mfupi. Kesho itakuwa siku ya kupumzika na kurejesha nguvu (recovery), kisha tutajipanga Jumatano na Alhamisi kabla ya kusafiri Ijumaa,” alisema Barker.

Kikosi kinatarajiwa kuwasili Malawi siku ya Ijumaa na kufanya mazoezi ya mwisho Ijumaa na Jumamosi kabla ya kuingia uwanjani.

Ingizo Jipya: Jabaar na Duchu Warejea

Habari njema kwa mashabiki wa Msimbazi ni kurejea kwa baadhi ya wachezaji waliokuwa nje kwa majeraha, jambo linaloongeza wigo mpana wa kikosi (depth).

Barker amethibitisha kuwa kiungo Ibraheem Jabaar yuko fiti kutumika, huku beki wa kulia David ‘Duchu’ Kameta akitarajiwa kuungana na timu kabla ya wikendi.

Mbinu za Barker na Mabadiliko ya Kikosi

Akizungumzia michezo iliyopita, Barker alikiri kukabiliwa na uhaba wa mabeki wa pembeni kutokana na majeraha na adhabu. Hali hiyo ilimlazimisha kumtumia beki wa kulia upande wa kushoto, beki wa kati kucheza pembeni, pamoja na kucheza bila kiungo halisi wa kukaba (defensive midfielder).

Licha ya mabadiliko hayo ya dharura, kocha huyo amewasifu wachezaji wake kwa kuonyesha ushujaa na kuondoka na pointi tatu muhimu.

Rekodi ya Ushindi 15 na Macho Kwenye CAF

Simba imeweka rekodi ya kushinda mechi 15 mfululizo za ligi (mechi 10 za msimu uliopita na 5 za msimu huu). Hata hivyo, Barker amesisitiza kuwa kwa sasa rekodi hiyo imewekwa pembeni ili kuangazia Ligi ya Mabingwa Afrika.

“Kipaumbele chetu cha kwanza ni kuvuka kizuizi hiki cha Mighty Wanderers, kabla ya kuanza kufikiria dabi na mechi zetu kubwa za ligi dhidi ya Azam FC na Yanga SC,” alihitimisha Barker.

Katwila Aweka Wazi Kilichoigharimu Geita Gold Mbele ya Simba SC Ukaribu wa Wifi na Shemeji: Fatma Mkambala Aweka Wazi Uhusiano Wake na Mke wa Jux, Priscilla Ojo