Katwila Aweka Wazi Kilichoigharimu Geita Gold Mbele ya Simba SC
KOCHA Mkuu wa Geita Gold FC, Zuber Katwila, amefunguka sababu zilizosababisha timu yake kupoteza pointi tatu muhimu dhidi ya Simba SC kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, akitaja makosa ya kimsingi wakati wa mabadiliko ya mpira (transition) na kushindwa kutumia nafasi.
Licha ya kipigo hicho, Katwila ameonyesha kuridhishwa na kiwango na nidhamu ya kiufundi iliyoonyeshwa na wachezaji wake uwanjani, akisisitiza kuwa timu yake ilicheza kulingana na mpango kazi waliojiwekea.
Makosa Ya Final Third Na Transition Yagharimu Geita Gold
Akizungumza baada ya mchezo huo, Katwila alieleza kuwa Geita Gold iliingia ikiwa inatambua vizuri ubora wa Simba SC, lakini changamoto kubwa ilikuwa kwenye eneo la mwisho la ushambuliaji (final third).
“Sisi tulikuwa bora zaidi yao leo uwanjani. Tulipaswa kumaliza mchezo salama, lakini tumepoteza. Mchezo ulikuwa mzuri kiufundi na tulijua tunacheza na timu ya aina gani, lakini wao walikuwa wajanja kwa kutumia nafasi zao,” alisema Katwila.
Mabao Yote Mawili Yalitokana na Nidhamu Ndogo
Katwila aliongeza kuwa mabao yote mawili yaliyofungwa na Simba SC yalitokana na makosa ya kurejea kwenye nafasi (defensive transition) mara baada ya timu yake kupoteza mpira.
“Magoli yote mawili yametoka kwenye transition. Walipata mpira, sisi tukawa out of position, wakafunga. Kama tungemaliza vizuri kwenye final third, hizo nafasi za wao kushambulia kwa kasi zisingetokea,” aliongeza kocha huyo.
Matumaini Mapya Kuelekea Michezo Inayofuata
Pamoja na matokeo hayo mabaya, Katwila anaamini mfumo na falsafa inayonyeshwa na kikosi chake inatoa picha nzuri kuelekea mechi zijazo za ligi. Anapanga kufanyia kazi safu ya ushambuliaji pamoja na nidhamu ya ulinzi wakati wa kupoteza mpira ili kuhakikisha wanapata matokeo chanya kwenye michezo inayofuata.