Farouk Komara Yanga
Yanga SC

Farouk Komara Aangaza Yanga: “Sitaki Maslahi Binafsi, Ni Timu Kwanza!”

Vardo September 1, 2026 9:55 am

Beki mpya wa Yanga SC, Farouk Komara, ameanza rasmi safari yake ndani ya kikosi hicho kwa kiwango cha juu, huku akiahidi kutoa mchango wake wote kwa ajili ya mafanikio ya timu badala ya kutanguliza maslahi binafsi.

Komara alipata fursa ya kuanza katika kikosi cha kwanza cha Yanga wakati mabingwa hao watetezi walipopata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Fountain Gate FC, kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa jijini Arusha.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Komara alisema alikuwa akisubiri kwa uvumilivu fursa hiyo na alipopata nafasi, aliamua kujituma kikamilifu ili kuisaidia timu kupata matokeo.

“Ilikuwa mechi nzuri sana. Nilikuwa ndani ya kikosi lakini nilikuwa nasubiri muda wangu. Leo wamenipa nafasi, hivyo ilipasa nitoe kila kitu kwa ajili ya timu na si kwa ajili yangu binafsi. Nilichotaka ni kuisaidia timu kupata ushindi,” alisema Komara.

Awasifu Mashabiki, Aangazia Kombe La Afrika

Beki huyo pia alitumia fursa hiyo kuwashukuru mashabiki wa Yanga waliojitokeza kwa wingi kuipa nguvu timu hiyo ugenini, akieleza kuwa ushirikiano wao unawapa hamasa kubwa wachezaji wakiwa uwanjani.

“Nawashukuru sana mashabiki kwa kuja kutuunga mkono, ni jambo zuri sana. Tumeshinda 2-0 ugenini, lakini tunapaswa kuendelea kupambana kwa sababu bado tuna mechi nyingi mbele yetu,” aliongeza.

Kiwango alichoonyesha Komara kinatoa ishara chanya kuelekea mechi zinazofuata, huku akibainisha kuwa akili yao sasa ipo kwenye michuano ya kimataifa.

“Mchezo unaofuata tutauingia kwa nguvu kama tunavyofanya kwenye mechi nyingine zote. Huu ni mchezo wa Kombe la Afrika, hivyo tutakabiliana nao kwa umakini wa hali ya juu na kuhakikisha tunafanya vizuri,” alitimisha.

Ukweli Kuhusu Kasi ya Shekhan Khamis Singida Black Stars: Yanga Walifanya Makosa? Barker Afichua Sababu ya Kumtoa Libasse Gueye Dhidi ya Geita Gold