Kocha Josiah Anena Baada ya Mashujaa FC Kurejea Kwenye Ushindi Ligi Kuu
BAADA ya kupata ushindi wa kwanza kwenye uwanja wa nyumbani kufuatia vipigo viwili mfululizo ugenini, Kocha Mkuu wa Mashujaa FC, Amani Josiah, amebainisha kuwa matokeo hayo yameongeza kujiamini na kuwapa nguvu mpya wachezaji wake.
Mashujaa FC hadi sasa imecheza mechi nne za Ligi Kuu Bara. Ilianza msimu kwa ushindi wa bao 1-0 ugenini dhidi ya Coastal Union, kabla ya kukumbana na vipigo viwili mfululizo ugenini kutoka kwa Fountain Gate (1-0) na Mbeya City (2-1). Hata hivyo, walirejea kwenye njia ya ushindi kwa kuichapa Kagera Sugar mabao 2-1 nyumbani.
Akizungumza kuhusu mchezo huo, Kocha Josiah alieleza kuwa haikuwa kazi rahisi kwani wapinzani wao walikuja kwa nia ya kusaka matokeo chanya, lakini kikosi chake kilionyesha nidhamu na roho ya kupambana.
“Tulijua haitakuwa rahisi kwa sababu wapinzani wetu walikuwa wametoka kupoteza ugenini, hivyo walikuja wakiwa na nia ya kubadilisha matokeo. Lakini wachezaji wangu walionyesha tabia nzuri ya kupambana. Pongezi kubwa ziende kwao kwa sababu walikuwa imara; tulikuwa nyuma lakini hawakukubali kuwa wanyonge, waliendelea kupambana na kutengeneza nafasi hadi tukapata ushindi,” alisema Josiah.
Kocha huyo aliongeza kuwa lengo lao kuu kwa sasa ni kutumia ushindi huo kama chachu ya kujenga mwendelezo mzuri wa matokeo kwenye mechi zinazofuata za ligi.
“Tunataka kutumia matokeo haya kutuweka vizuri zaidi. Ushindi kama huu unaongeza kujiamini ndani ya kikosi, lakini tunatakiwa kuutumia kama mwanzo wa kujenga mambo mazuri zaidi kwenye mechi zinazofuata,” alisisitiza.
Kibarua kinachofuata kwa Mashujaa FC kitakuwa ugenini dhidi ya Dodoma Jiji, mchezo utakaopigwa Septemba 4, 2026, kuanzia saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.