Datius Peter Geita Gold
Michezo

Datius Peter Afunguka Siri ya Kutokuhofia Wachezaji Wakubwa Ligi Kuu

Vardo September 3, 2026 1:23 pm

Beki wa kati wa Geita Gold, Datius Peter, amesema hana shaka wala presha anapokutana na wachezaji wenye majina makubwa na ubora wa juu uwanjani, akieleza kuwa uzoefu wake wa miaka tisa katika Ligi Kuu Bara umemjengea kujiamini na uwezo mkubwa wa kukabiliana na changamoto yoyote.

Datius, ambaye amewahi kuzitumikia klabu za Stand United, Mbao FC, Kagera Sugar na Mtibwa Sugar kabla ya kujiunga na Geita Gold, alibainisha hayo mara baada ya kumalizika kwa mchezo wa Ligi Kuu Bara ambapo timu yake ilipoteza kwa mabao 2-0 dhidi ya Simba SC.

Akizungumzia ugumu wa mchezo huo, Datius alikiri kuwa ubora na kasi ya mawinga wa Simba viliwapa changamoto uwanjani, lakini akasisitiza kuwa makosa binafsi waliyofanya wao wenyewe ndiyo yaliyowagharimu na kuwapa ushindi wapinzani wao.

“Sipati presha yoyote kwa sababu najiamini na uzoefu ninao. Nikikutana na mpinzani wangu naona ni jambo la kawaida tu kama ninavyokutana na wachezaji wengine, ila lazima nimpe heshima yake uwanjani,” alisema Datius.

Beki huyo aliongeza kuwa matokeo hayo hayajawakatisha tamaa au kuwapa presha kubwa, bali yamewapa somo la kujirekebisha ili kufanya vizuri zaidi kwenye mechi zinazofuata za Ligi Kuu.

Geita Gold, iliyorejea Ligi Kuu Bara msimu huu, imeshacheza mechi tano ambapo imeshinda mbili, ikapoteza mbili na kutoka sare mchezo mmoja. Hivi sasa imekusanya pointi saba na kushika nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi.

Cesc Fàbregas Atwaa Tuzo ya Kocha Bora Serie A