Juana Ortegon: Nahodha wa Colombia Atangaza Vita Kombe la Dunia U-20
NAHODHA wa timu ya taifa ya wanawake ya Colombia ya umri chini ya miaka 20, Juana Ortegon, ameweka wazi kuwa kikosi chao hakina lengo jingine zaidi ya kupambana hadi mwisho na kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia la Wanawake la U-20 litakalofanyika nchini Poland.
Ortegon mwenye umri wa miaka 20, ambaye pia ni kiungo mwenye ushawishi mkubwa katika klabu ya Independiente Santa Fe, amekabidhiwa kitambaa cha unahodha kufuatia uzoefu wake mrefu katika mashindano ya kimataifa ya vijana.
Safari ya nyota huyu ilianza tangu akiwa na umri wa miaka 15, ambapo alishiriki Kombe la Dunia la Wanawake la U-17 mwaka 2022. Baadaye aliendelea kuwa nguzo muhimu katika kikosi cha Colombia cha U-20 kwenye michuano ya mwaka huo huo na ile ya mwaka 2024 iliyofanyika nchini kwao.
Akizungumzia malengo ya timu hiyo, Ortegon alisema:
“Malengo yetu ni kubeba taji. Tayari tumepata uzoefu wa kutosha kwenye mashindano makubwa, kilichobaki sasa ni kulinyanyasa taji hilo na tunaamini msimu huu inawezekana.”
Aliongeza kuwa safari yake ya soka imemsaidia kukua sio tu kama mchezaji, bali pia katika uongozi na namna ya kukabiliana na presha kubwa ya mashindano ya kiwango cha kimataifa.
Katika michuano iliyopita ya mwaka 2024 iliyofanyika nchini kwao, Colombia iliishia hatua ya robo fainali baada ya kuondolewa na Uholanzi kwa mikwaju ya penati 3-0 kufuatia sare ya 2-2. Ortegon anaamini mafunzo waliyoyapata pale yatakuwa chachu ya kufanya vyema zaidi Poland.
Katika Kombe la Dunia la U-20 linalokuja, Colombia imepangwa Kundi E pamoja na mataifa ya Costa Rica, Korea Kaskazini na Ureno.
Kikosi hiki cha Colombia kinarajiwa kuendeleza moto uliowashwa na nyota wakubwa wa nchi hiyo kama Linda Caicedo, Mayra Ramirez, na Leicy Santos ambao kwa sasa wanakipiga katika timu ya wakubwa.