Steve Barker Aitahadharisha Mighty Wanderers: Simba Tuko Tayari Ligi ya Mabingwa!
KOCHA Mkuu wa Simba SC, Steve Barker, amesisitiza kuwa kikosi chake kipo kwenye hali ya juu ya maandalizi kuelekea mchezo wa kwanza wa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Mighty Wanderers ya nchini Malawi.
Mchezo huo unachezwa leo nchini Malawi, huku Simba ikiwa na lengo moja pekee: kupata matokeo chanya ugenini ili kutengeneza mazingira mazuri kabla ya mchezo wa marudiano utakaopigwa jijini Dar es Salaam.
Barker ameeleza kuwa benchi la ufundi na wachezaji wanatambua uzito wa mashindano ya kimataifa, hivyo wamejipanga vizuri kiufundi na kisaikolojia ili kuanza safari yao vizuri.
“Ligi ya Mabingwa ni mashindano yenye hadhi kubwa barani Afrika. Kila timu inataka kufanya vizuri, na Simba tukiwa miongoni mwa klabu kubwa, tumejiandaa kikamilifu kwa changamoto hii,” alisema Barker.
Heshima Kwa Mighty Wanderers Pamoja na matumaini makubwa waliyonayo, Kocha Barker ameweka wazi kuwa hawawadharau wapinzani wao, kwani timu yoyote inayoshiriki mashindano haya inastahili heshima.
Amebainisha kuwa Mighty Wanderers ina wachezaji wenye uzoefu, wakiwemo wanaoitumikia timu ya taifa, jambo linalowafanya Simba kuingia uwanjani kwa umakini mkubwa.
“Kucheza mechi za Afrika ugenini kamwe si kazi rahisi. Tunaiheshimu Mighty Wanderers kwa sababu ni timu bora iliyofanya vizuri msimu uliopita. Lakini heshima hiyo haitutoe kwenye msingi wetu wa kusaka ushindi,” aliongeza.
Lengo Ni Hatua ya Makundi na Zaidi Barker amebainisha kuwa malengo ya Simba SC si kuishia hatua za awali, bali ni kufika mbali zaidi katika mashindano ya msimu huu, ikiwemo kutinga hatua ya makundi na kuwania mataji.
Amesisitiza kuwa morali ya wachezaji ipo juu na kila mmoja ana hamu ya kuingia uwanjani kuipigania nembo ya Simba SC.