Cyprian Kachwele Ajiunga na Kryvbas ya Ukraine Kwa Mkataba wa Miaka 4
MSHAMBULIAJI kijana na nyota wa kimataifa wa Tanzania, Cyprian Kachwele, ametambulishwa rasmi na klabu ya Kryvbas Kryvyi Rih inayoshiriki Ligi Kuu nchini Ukraine.
Kachwele (21) amejiunga na miamba hiyo kama mchezaji huru kwa mkataba wa miaka miwili baada ya kukamilisha mkataba wake na Vancouver Whitecaps ya Canada. Msimu uliopita, alikuwa akicheza kwa mkopo katika klabu ya HFX Wanderers ya Canada, ambapo alionyesha kiwango cha kuridhisha na kujiongezea uzoefu mkubwa.
Chachu Mpya Kwenye Safu ya Ushambuliaji
Kryvbas, ambayo ilimaliza msimu uliopita katika nafasi ya saba ikiwa na pointi 48 na kufunga mabao 53 kwenye michezo 30, inatarajiwa kufaidika kwa kiasi kikubwa na usajili huu. Uwezo wa Kachwele wa kucheza kama mshambuliaji wa kati (center-forward), pamoja na matumizi yake mazuri ya nguvu na urefu eneo la hatari, utaongeza ubora na utofauti kwenye safu yao ya ushambuliaji.
Safari Yake ya Soka: Kutoka Azam FC Mpaka Ulaya
Safari ya mafanikio ya Kachwele ilianzia katika akademi ya Azam FC mwaka 2023 kabla ya kupandishwa kikosi cha kwanza. Badae alitimkia Canada kujiunga na Vancouver Whitecaps FC 2 inayoshiriki MLS NEXT Pro.
Akiwa na Vancouver Whitecaps FC 2, Kachwele alicheza jumla ya mechi 39, akifunga mabao 11 na kutoa asisti mbili:
-
Msimu wa 2024: Alicheza mechi 20, akafunga mabao 4 na kutoa asisti 1.
-
Msimu wa 2025: Alionyesha kiwango cha juu zaidi akicheza mechi 19, akifunga mabao 7 na kutoa asisti 4.
Kiwango chake bora kilimwezesha kupata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza cha Vancouver Whitecaps kwenye Ligi Kuu ya Marekani (MLS), ambapo alipata nafasi ya kuanza kwenye baadhi ya mechi.
Hatua Mpya Kwenye Timu ya Taifa
Usajili huu unakuja wakati muafaka kwani Kachwele amejumuishwa kwenye kikosi cha Timu ya Taifa (Taifa Stars) kinachojiandaa na mechi za kufuzu AFCON 2027 dhidi ya Guinea-Bissau na Madagascar, pamoja na mchezo wa kirafiki dhidi ya Ghana.
Kwa kujiunga na Kryvbas, Kachwele anakuwa mtanzania mwingine kufuata nyayo za Novatus Miroshi aliyewahi kucheza Ligi Kuu ya Ukraine akiwa na miamba ya Shakhtar Donetsk.