Yanga vs Gaborone United
Yanga SC

Yanga vs Gaborone United: Ali Kamwe Aweka Wazi Mbinu ya Ushindi na Bouncer la Mashabiki

Vardo September 8, 2026 5:31 pm

Msemaji wa Yanga, Ali Kamwe, ametoa wito mzito kwa mashabiki wa klabu hiyo kujitokeza kwa wingi kwenye mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Gaborone United ya Botswana, akisisitiza kuwa hamasa ya mashabiki ndiyo itakayochochea kasi ya ushindi mapema.

Yanga inajiandaa kuwa mwenyeji wa Gaborone United Siku ya Jumamosi kwenye Uwanja wa Azam Complex, ikiwa na lengo moja tu: kupata matokeo chanya ili kukata tiketi ya kusonga mbele katika mashindano hayo makubwa barani Afrika.

Ubora na Hatari ya Gaborone United Akishusha tathmini yake kuhusu mpinzani wao, Kamwe ameeleza kuwa Gaborone United si timu ya kuogopwa, ingawa wana hatari kubwa wanapopata mipira iliyokufa (set-pieces) kama vile kona na faulo.

“Si mchezo wa kutisha, ni mchezo wa kawaida tu. Lakini quality ya Gaborone ipo kwenye maeneo hatari—hasa kwenye set pieces. Muda wowote wanaweza kupata kona au free kick na kuitumia vizuri,” alisema Kamwe.

Mbinu ya Kuwamaliza Mapema Ili kudhibiti hatari hiyo, Kamwe ameeleza kuwa benchi la fundi na wachezaji wanapaswa kuanza mchezo kwa kasi kubwa ili kupata mabao ya mapema na kuondoa kabisa presha ya wapinzani wao.

“Ni lazima tukabiliane na mpinzani wa namna hii kwa kumpelekea moto mapema. Dakika za mwanzo tupate matokeo mazuri ili tuweze kupunguza madhara yao,” aliongeza.

Nguvu ya Mashabiki na “Mafuriko” Azam Complex Msemaji huyo alisisitiza kuwa sauti na mwamko wa mashabiki jukwaani utawapa wachezaji nguvu ya ziada huku ukiongeza presha kwa wageni.

“Tukitokeza kwa pamoja pale Azam Complex, tukajae kwa wingi na kuwa-push wachezaji wetu, dakika za mapema tutakuwa tumeshamaliza hii match. Wazofisha hawa ni mafuriko! Na mafuriko kwenye mpira huanzia kwa mashabiki,” alisema kwa kujiamini.

Tahadhari ya Mzaha Uwanjani Pamoja na kujiamini huko, Kamwe aliwatahadharisha wachezaji na mashabiki kutochukulia mchezo huo kwa mzaha au kuudharau mpinzani.

“Tukicheza-cheza tu pale na kuleta mzaha tukisema jambo hili ni jepesi, tutawapa nafasi. Mpira mmoja tu wa kutengua unaweza kuwafanya watuadhibu na shughuli ikawa ngumu hapa.”

Kamwe alihitimisha kwa kuwaomba mashabiki kuendelea kuiamini timu yao na kuwa sehemu ya ushindi kwa kujitokeza kwa wingi kutoa hamasa kuanzia dakika ya kwanza.

Icy Fruits Yaingia Uwanjani Kukupa Barafu Na Matunda Chama Azungumzia Mechi ya Marudiano Simba vs Mighty Wanderers CAF Champions League