Clara Luvanga
Habari za michezo

Clara Luvanga Aweka Rekodi ya Dunia: Asajiliwa Washington Spirit Kwa Sh5.2 Bilioni

Vardo September 12, 2026 6:04 pm

Mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Clara Luvanga, ameweka historia mpya duniani baada ya kukamilisha uhamisho wake kutoka Al Nassr ya Saudi Arabia kwenda Washington Spirit inayoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake nchini Marekani (NWSL).

Uhamisho huo wa mkataba wa miaka minne umegharimu ada ya Euro 1.7 milioni (takriban Sh5.2 bilioni), hatua inayomfanya Luvanga kuwa mchezaji ghali zaidi katika historia ya soka la wanawake duniani kwa sasa.

Rekodi hiyo awali ilikuwa ikishikiliwa na Grace Geyoro, aliyehamia London Lionesses kutoka PSG kwa ada ya Euro 1.65 milioni (Sh5 bilioni) mnamo Septemba 2025.

Orodha ya Wachezaji 5 Ghali Zaidi Soka la Wanawake Duniani:

  1. Clara Luvanga (Al Nassr kwenda Washington Spirit) – Euro 1.7M (Sh5.2 Bilioni)

  2. Grace Geyoro (PSG kwenda London Lionesses) – Euro 1.65M (Sh5 Bilioni)

  3. Kerolini Nicole (Manchester City kwenda Barcelona) – Euro 1.5M (Sh4.6 Bilioni)

  4. Felicia Schröder (BK Hacken kwenda Real Madrid) – Euro 1.5M (Sh4.6 Bilioni)

  5. Lizbeth Ovalle (Tigres UANL kwenda Orlando Pride) – Euro 1.3M (Sh4 Bilioni)

Kiwango cha juu cha ufungaji alichokionyesha Luvanga, ambaye pia aliwahi kuichezea Yanga Princess na DUX Logroño ya Hispania, kimekuwa chachu kuu ya Washington Spirit kuwekeza kiasi hicho kikubwa cha fedha ili kunasa saini yake.

Akizungumza baada ya kutambulishwa, Luvanga (21) alieleza furaha yake ya kuanza maisha mapya Marekani:

“Nina furaha sana kujiunga na Washington Spirit na kukabiliana na changamoto hii mpya katika NWSL. Najua nimewasili wakati msimu ukiwa unaendelea, lakini nina hamu kubwa ya kuisaidia timu kufanya vizuri kuelekea hatua ya mchujo (playoffs). Go Spirit!”

Akiwa na Al-Nassr, Luvanga alitwaa mataji matatu mfululizo ya ligi kuu, Kombe la Wanawake la Saudi Arabia, Super Cup, na Mashindano ya Klabu za Wanawake ya WAFF 2026. Msimu wa 2025/26 ulikuwa wa mafanikio makubwa kwake, ambapo alishinda Kiatu cha Dhahabu baada ya kupachika mabao 24 katika mechi 14 pekee.

KVZ vs Asswehly: Hababuu Ali Abadili Mbinu Kusaka Ushindi Zanzibar