KVZ vs Asswehly: Hababuu Ali Abadili Mbinu Kusaka Ushindi Zanzibar
Kocha Mkuu wa KVZ, Hababuu Ali, amethibitisha kubadili mfumo na mbinu za uchezaji kuelekea mchezo wao wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Asswehly ya Libya, akisisitiza kuwa safu yake ya ushambuliaji itapambana kusaka ushindi wa mabao 2-0.
Mchezo huo unatarajiwa kupigwa kesho Jumapili kuanzia saa 10:00 jioni katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar. KVZ wana kibarua cha kupindua matokeo baada ya kufungwa bao 1-0 katika mchezo wa kwanza uliochezwa nchini Libya.
Mbinu Mpya na Mipango ya Ushindi
Kocha Hababuu ameeleza kuwa nidhamu ya kuzuia waliyoonyesha ugenini ilikuwa na lengo la kuepuka kufungwa idadi kubwa ya mabao, na sasa ni wakati wa kushambulia kikamilifu.
“Tulipokwenda Libya tulitumia mfumo wa kujilinda zaidi kwa sababu tulikuwa ugenini na tulitaka kupunguza madhara. Kufungwa 1-0 kunatupa nafasi nzuri ya kurekebisha makosa tukiwa nyumbani. Safari hii tunakwenda kushambulia ili kupata mabao 2-0 na kufuzu hatua inayofuata,” alisema Hababuu.
Ameongeza kuwa mechi za kimataifa zimekuwa fursa nzuri ya kuijenga timu na kufanya tathmini ya mara kwa mara ili kuboresha kikosi chake.
Hali ya Kikosi na Wachezaji Wasiokuwepo
Katika mchezo huo wa marudiano, KVZ itakosa huduma ya wachezaji wawili muhimu kutokana na majeraha:
-
Abdallah Idd Mtumwa ‘Pina’
-
Samir Caragher
Nahodha wa KVZ, Bashir Muslim Darwesh ‘Iker’, amewatoa hofu mashabiki na kueleza kuwa kikosi kipo tayari kurekebisha makosa yote yaliyojitokeza kwenye mechi ya kwanza ili kuondoka na ushindi mnono nyumbani.
Hamasisho na Kiingilio Bure Uwanjani
Katibu wa Kamati ya Habari na Masoko wa Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF), Mohamed Kabwanga, ametoa wito kwa mashabiki kujitokeza kwa wingi kuipa sapoti timu hiyo ya nyumbani.
Hamasa hiyo imeongezwa na Mkuu wa Kikosi cha Valantia Zanzibar, Luteni Kanali Said Shamhuna, ambaye amenunua tiketi 15,000 ili kuruhusu mashabiki kuingia uwanjani bure. Uwanja wa New Amaan Complex una uwezo wa kuchukua mashabiki 15,000, hivyo mashabiki wote watapata fursa ya kushuhudia pambano hilo bila malipo.