Mangungu Simba SC
Simba SC

Mangungu Aitumia Ujumbe Mzito Afrika Baada ya Simba Kushinda 6-1

Vardo September 14, 2026 10:25 am

MWENYEKITI wa Simba SC, Murtaza Mangungu, ametoa onyo kali kwa klabu za Afrika baada ya timu hiyo kuibuka na ushindi mnono wa mabao 6-1 dhidi ya Mighty Wanderers ya Malawi, akisisitiza kuwa sasa hivi ni muda wa vitendo kuzungumza na si maneno.

Ushindi huo wa kishindo katika mchezo wa marudiano uliopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, uliifanya Simba kufuzu hatua inayofuata ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa ushindi wa jumla wa mabao 7-1, kufuatia ushindi wa bao 1-0 ugenini Lilongwe, Malawi.

“Tuliwafunga Uwanjani na Mdomoni”

Akizungumzia matokeo hayo, Mangungu alisema kuwa maneno ya kanda mbili yaliyotolewa na wapinzani wao kabla ya mchezo yaliwaongezea hamasa kubwa ya kupata matokeo ya kishindo nyumbani.

“Umekwisha vizuri kwa maana tumeshinda. Ushindi wetu si kwamba tulitaka kuwadhalilisha, lakini walichokisema kupitia vyombo vya habari kilitupa hamasa. Ukitoka kwenda kwenye mechi ya watu halafu unapita kwenye vyombo vya habari ukitamba, basi tumewafunga uwanjani na tumewafunga midomo vilevile,” alisema Mangungu.

Mwenyekiti huyo alieleza kuwa mchezo wa kwanza nchini Malawi ulikuwa wa hesabu kutokana na ubovu wa uwanja, lakini benchi la ufundi lilifanya marekebisho ya kiufundi yaliyoleta matunda Dar es Salaam.

Pongezi kwa Benchi la Ufundi na Serikali

Mangungu alipongeza benchi la ufundi na wachezaji kwa kiwango cha juu walichoonyesha, huku akitoa shukrani kwa Serikali kwa kuwezesha matumizi ya Uwanja wa Uhuru pamoja na mashabiki waliojitokeza kwa wingi kuipa timu hamasa.

“Hii ndiyo maana halisi ya Simba. Tumekuwa tukisema mara zote kuwa vitendo vinaongea zaidi ya maneno. Mpira hauchezwi kwa maneno ya pembeni, unachezwa uwanjani. Hata hivyo, tungeweza kufunga mabao mengi zaidi kama tungetumia nafasi zote tulizotengeneza,” aliongeza.

Gueye Apongezwa, Mashabiki Waonywa

Kuhusu kiwango cha mshambuliaji Libasse Gueye aliyefunga mabao mawili, Mangungu alisema Mighty Wanderers walifanya kosa kubwa kumfanya mchezaji huru kwa kuzingatia nyota wengine wa Simba, jambo lililompa nafasi Senegali huyo kuonyesha cheche zake.

Hata hivyo, Mangungu aliwataka mashabiki wa Simba kuwa na mpango wa muda mrefu na kutotarajia ushindi wa mabao mengi katika kila hatua.

“Kila hatua kwenye michuano ya kimataifa inakuwa ngumu zaidi. Lengo letu kuu ni kusonga mbele na kujenga timu itakayoshindana na vigogo wa Afrika, si tu kufunga mabao mengi kila mchezo,” alihitimisha Mangungu.

Barker Afichua Siri ya Simba Kuilaza Wanderers 6-1, Aitishia Azam FC Simba SC Yocha Mighty Wanderers 6-1: Mkwabi Aagiza Azam FC Wakae Tayari!