Simba SC vs Mighty Wanderers
Simba SC

Barker Afichua Siri ya Simba Kuilaza Wanderers 6-1, Aitishia Azam FC

Vardo September 14, 2026 10:16 am

Kocha Mkuu wa Simba SC, Steve Barker, amesema ushindi mnene wa mabao 6-1 dhidi ya Mighty Wanderers ya Malawi haukuwa wa bahati, bali ulikuwa mpango mkakati wa timu yake kuanza mchezo kwa kasi kubwa na presha ya juu.

Simba ilionyesha utawala wa hali ya juu katika mchezo huo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika uliopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam. Wekundu hao wa Msimbazi walipachika mabao matatu kipindi cha kwanza kabla ya kuongeza mengine matatu kipindi cha pili, na kufanya matokeo ya jumla kuwa ushindi wa 7-1.

Akizungumza baada ya mechi hiyo, Barker alieleza kuwa ujumbe wake kwa wachezaji wakati wa mapumziko ulikuwa ni kuendeleza kasi bila kuwapa nafasi wapinzani kurejea mchezoni.

“Si mara nyingi unaona matokeo makubwa kama haya, lakini tulivyoanza na kufunga mabao matatu mapema ilikuwa mwanzo mzuri. Wakati wa mapumziko niliwaambia wachezaji tusipunguze kasi. Nilihisi kabisa huu ulikuwa mchezo wa kupata mabao matano au sita,” alisema Barker.

Libasse Gueye na Chama Wapewa Maua Yao

Barker hakusita kumwagia sifa mshambuliaji wake, Libasse Gueye, kwa kuisumbua safu ya ulinzi ya Wanderers, akimwezea kama mchezaji mwenye uwezo mkubwa wa kushambulia moja kwa moja na kuwavuruga mabeki.

Pia alimsifu Clatous Chama kwa kufunga bao la mapema, akibainisha kuwa uzoefu wake na uwezo wa kucheka na nyavu ni miongoni mwa silaha kuu za Simba msimu huu.

“Tulidhibiti mchezo kupitia umiliki mzuri wa mpira. Hali hiyo iliwafanya wapinzani wachoke na kutuachia mianya tuliyoitumia vizuri,” aliongeza kocha huyo.

Wachezaji wa Akiba Waonyesha Ubora

Kocha huyo alieleza kufurahishwa na mchango wa Kalesto Makgalwa na Maurice walioingia kutokea benchi na kuhusika moja kwa moja kwenye bao la mwisho. Kalesto alifunga na kutoa pasi ya bao (assist), huku Maurice akihitimisha karamu hiyo ya mabao kwa shuti safi.

Kibarua Kipya Dhidi ya Azam FC

Pamoja na ushindi huo mkubwa, Barker amesisitiza kuwa Simba haina muda wa kusherehekea kwani akili zote zimehamia kwenye mchezo ujao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam FC utakaopigwa Jumatano.

Barker amebainisha kuwa lengo lao ni kudumisha rekodi ya ushindi wa asilimia 100 kwa kushinda michezo yote sita ya kwanza ya ligi hiyo.

Simba SC Yaichapa Mighty Wanderers 6-1, Yatinga Hatua Inayofuata Ligi ya Mabingwa Afrika Mangungu Aitumia Ujumbe Mzito Afrika Baada ya Simba Kushinda 6-1