Steve Barker Aweka Wazi Siri ya Mafanikio Simba SC na Mchango wa Mo Dewji
Kocha Mkuu wa Simba SC, Steve Barker, ameweka wazi siri inayokipa klabu hiyo uwezo wa kufanya maandalizi ya kiwango cha juu, huku akimtaja Rais na Mwekezaji wa klabu hiyo, Mheshimiwa Mohammed Dewji ‘Mo’, kuwa nguzo kuu ya mafanikio hayo.
Barker ameeleza kuwa uwezo wa Simba kuweka kambi za maandalizi nje ya nchi na kusafirisha kikosi kizima—ikijumuisha wachezaji, benchi la ufundi na wafanyakazi wengine—unatokana na uwekezaji mkubwa wa rasilimali kutoka kwa Mo Dewji.
“Unajua si jambo rahisi kusafiri nje ya nchi na wachezaji wote, benchi la ufundi na wafanyakazi wote wa timu. Inahitaji rasilimali nyingi sana kuweza kufanya jambo kama hili,” alisema Barker.
Kocha huyo aliongeza kuwa tangu siku yake ya kwanza kuwasili Msimbazi, Dewji amekuwa akitoa ushirikiano wa karibu na sapoti isiyo na kifani. Mawasiliano yao ya mara kwa mara yamekuwa nguzo muhimu katika kuhakikisha timu inapata kila inachohitaji kwa ajili ya ushindani.
“Tangu siku ya kwanza nilipowasili klabuni, Rais wetu, Mheshimiwa Dewji, ameisaidia timu kwa kiwango kikubwa sana. Ninaongea naye mara kwa mara. Ni mtu mwenye mapenzi makubwa sana na Simba Sports Club. Anatoa muda wake mwingi na rasilimali zake kwa ajili ya timu,” alisisitiza Barker.
Aidha, Barker alibainisha kuwa sapoti hiyo haishii tu kwenye kambi za nje ya nchi, bali hata wanapokuwa nyumbani Tanzania, mahitaji yote ya kiufundi yanayoombwa yamekuwa yakipatiwa majibu kwa haraka.
Akitamatisha, Kocha Barker alisisitiza kuwa jukumu la wachezaji na benchi la ufundi ni kulipa uwekezaji huo kwa matokeo chanya uwanjani. Alieleza kuwa njia pekee ya kumshukuru Mo Dewji kwa imani na nguvu anayoweka ni kuhakikisha timu inajiandaa kwa ubora wa hali ya juu na kupata ushindi kwenye michezo yao.