Simba Queens vs Yanga Princess Leo: Vita ya Kukata na Shoka Ngao ya Jamii Wanawake
Pazia la msimu mpya wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara (WPL) linafunguliwa rasmi leo, Septemba 30, kwenye Uwanja wa KMC, Mwenge jijini Dar es Salaam, kwa mechi mbili za nusu fainali ya Ngao ya Jamii.
Kipute hiki cha Ngao ya Jamii kinazikutanisha timu nne zilizomaliza nafasi za juu msimu uliopita, kikiwa na dabi mbili zenye msisimko wa pekee: dabi ya kijeshi kati ya JKT Queens na Mashujaa Queens, pamoja na Dabi ya Kariakoo inayowakutanisha mabingwa watetezi Simba Queens dhidi ya Yanga Princess.
Macho na masikio ya mashabiki wengi yataelekezwa kwenye Dabi ya Kariakoo, ambapo miamba hii miwili itachuana vikali kusaka tiketi ya kucheza fainali.
Rekodi za Timu na Historia
Simba Queens wanaingia kwenye mchezo huu wakiwa na jeuri ya mabingwa watetezi wa Ligi Kuu na ubora wa kimbinu waliojenga kwa miaka kadhaa. Wekundu wa Msimbazi wamekuwa na utulivu mkubwa kwenye mechi za presha, wakijivunia rekodi nzuri ya ushindi dhidi ya watani wao wa jadi.
Tangu kuanzishwa kwa mashindano haya mwaka 2023, Simba Queens imetwaa taji hili mara moja (2023), huku JKT Queens wakinyakua mara mbili mfululizo (2024 na 2025). Tangu wakati huo, Simba na Yanga zimekutana mara tatu; mechi mbili zikimalizika kwa sare na moja Simba wakiondoka na ushindi.
Kwa upande wa Yanga Princess, wanaingia uwanjani wakiwa na shauku kubwa ya kufuta unyonge na kuonyesha mageuzi makubwa yaliyofanyika kwenye kikosi chao kupitia usajili wa msimu huu.
Vita ya Kiungo: Eneo Litakaloamua Mchezo
Mchezo huu unatarajiwa kuamuliwa katikati ya uwanja, ambapo mbinu, ubunifu na nguvu vitakutana face-to-face:
-
Simba Queens: Wanajivunia safu ya kiungo iliyokaa pamoja kwa muda mrefu, jambo linalowapa faida ya kuelewana (chemistry). Wachezaji kama Elizabeth Mkuki, Vivian Corazone, Elizabeth Wambui na Brice Zanga wanatoa utulivu wa kumiliki mpira na kupanga mashambulizi. Corazone na Zanga watakuwa na kazi ya kukabili mashambulizi, huku Mkuki na Wambui wakipika mabao.
-
Yanga Princess: Wanakuja na sura mpya na nguvu mpya. Wanamtegemea Mkenya Agnes Pallangyo mwenye uzoefu wa ligi ya ndani, akisaidiwa na Joanita Nabirye (kutoka Uganda) pamoja na Tems Getanga (aliyetokea CBE ya Ethiopia). Mchanganyiko huu unawapa Yanga nguvu na ufundi wa kushindana kimwili na kuzuia utawala wa Simba.
Safu za Ushambuliai: Nani Mkali wa Mabao?
Pande zote mbili zimefanya mabadiliko makubwa kwenye safu zao za ushambuliaji:
-
Simba Queens: Bado wanamkosa mfungaji wao hatari Jentrix Shikangwa aliyetimkia FC Masar ya Misri. Hata hivyo, wamemsajili Senaf Semise (kutoka CBE ya Ethiopia)—aliyekuwa mfungaji bora wa CECAFA 2024 akiwa na mabao 6. Safu hii pia imeongezewa nguvu na Mary Siyame (Fountain Gate Princess) na Rida Kusamfulla kutoka Cameroon.
-
Yanga Princess: Wanamtegemea Sandrine Mutuyimana kutoka Inyemera WFC ya Rwanda (aliyesajiliwa kuziba nafasi ya Jeaninne Mukandayisenga aliyetimkia China). Mutuyimana, aliyefunga mabao 10 msimu uliopita, atashirikiana na Rehema Ramadhan na winga machachari Winifrida Charles kuunda safu yenye kasi ya kushambulia kwa kushtukiza.
Mbinu na Kauli za Makocha
Nusu fainali hii itaamuliwa na utulivu wa kiungo, umakini wa safu za ulinzi, na mbinu za makocha wote wawili: Mussa Hassan ‘Mgosi’ wa Simba Queens na Edna Lema wa Yanga Princess.
Kocha Mussa Hassan ‘Mgosi’ (Simba Queens): “Tunajua hii ni dabi na ina heshima yake. Tunaingia tukiwaheshimu wapinzani wetu, lakini tunaamini tutafanya vizuri kwa sababu tulijiandaa vyema.”
Nahodha Fatuma Mustafa (Mashujaa Queens): “Tumejiandaa vizuri kucheza na JKT ambayo ni timu ngumu. Tupo tayari kupambana na kuhakikisha tunapata matokeo mazuri.”