Taarifa Njema Yanga SC: Kamwe Afunguka Hali ya Wachezaji Kambini
Klabu ya Yanga SC imeanza rasmi kurejea kwenye programu zake za maandalizi baada ya mapumziko mafupi, huku ikitoa taarifa njema na ya kutuliza mioyo ya mashabiki kuhusu hali ya wachezaji wa Yanga waliorejea kambini.
Akimwaga nondo kuhusu maandalizi hayo, Msemaji wa Yanga, Ali Kamwe, ameeleza kuwa nyota waliobaki baada ya wenzao 15 kuitwa kwenye majukumu ya timu za Taifa, wameripoti kambini wakiwa katika utimamu mkubwa wa mwili na afya njema.
“So far, kwa sababu kuna wachezaji wengi, takriban wachezaji 15 wapo kwenye majukumu ya timu za Taifa. Lakini wale waliobaki tuko nao hapa na leo wameripoti siku ya kwanza, wapo kwenye condition nzuri,” amesema Kamwe.
Hamna Majeraha Mapya Kambini
Moja ya mambo yaliyowapa furaha benchi la ufundi ni kutopokea taarifa za majeraha yoyote mapya. Kamwe amebainisha kuwa nidhamu ya wachezaji na ufuatiliaji wa karibu kutoka kwa timu ya wataalamu wa mazoezi (fitness team) wakati wa mapumziko imesaidia sana kuzuia majeraha.
Kamwe amefafanua:
“Hatujapokea mchezaji yeyote ambaye amepata injury katika kipindi hiki cha mapumziko na wote wamerudi, afya zao ziko salama. Good thing ni kwamba wamerudi wakiwa kwenye shape nzuri kwa sababu timu yetu ya fitness ilikuwa inafuatilia programs zao.”
Wamerudi Kwenye Tempo Nzuri
Ufuatiliaji huo wa karibu umeiwezesha timu kuanza mazoezi kwa kasi ya juu bila kuhitaji muda mrefu wa kurejesha utimamu wa mwili (fitness level).
“Wamerudi kwenye tempo nzuri. Kwa hiyo ni kutoa mashaka kwa mashabiki na wapenzi wa klabu wetu ya Young Africans, simply we are back, tumerudi katika ubora wetu,” amesisitiza Kamwe.
Ingawa benchi la ufundi linaendelea na mazoezi likiwa na idadi ndogo ya wachezaji huku likisubiri nyota 15 waliopo timu za Taifa kuungana nao, hali ya utulivu na ubora wa waliopo unatoa picha nzuri kuelekea michezo ijayo ya ligi na kimataifa.