Simba Queens Yaikandika Yanga Princess: Ahmed Ally Afunguka Makubwa
Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, amemwaga cheche baada ya Simba Queens kuendeleza ubabe na kuiondoa Yanga Princess kwenye hatua ya nusu fainali ya Ngao ya Jamii ya Ligi ya Wanawake Tanzania na kutinga fainali kwa kishindo.
Akizungumza mara baada ya mchezo huo, Ahmed Ally alisema ushindi huo ni thibitisho tosha la tofauti kubwa ya kiwango iliyopo kati ya timu hizo mbili kwenye soka la wanawake nchini, akisisitiza kuwa Yanga Princess bado wapo mbali sana kufikia mafanikio ya Simba Queens.
“Tuko mbali sana kwenye soka la wanawake. Yanga Princess wanajitahidi kutusogelea, lakini kila wakijaribu kufanya hivyo, sisi tunawadidimiza chini zaidi ili wasisogee kabisa kwenye anga zetu,” alisema Ahmed Ally.
“Hatuwapi Nafasi Hata Kidogo” — Ahmed Ally
Ahmed aliongeza kuwa Simba Queens haina mpango wa kuwapa mpenyo wapinzani wao katika vita yoyote ya ubingwa, kwani msimamo wa klabu hiyo ni kuendelea kutawala soka la wanawake na kuzuia Yanga Princess kupata mafanikio yoyote.
“Inapokuja kwenye vita yoyote ya ubingwa, hatumpi nafasi hata kidogo. Hatumuachi achukue ubingwa hata mmoja, sababu hatutaki apate mafanikio hata kwa sekunde moja,” alisisitiza kiongozi huyo.
Mchango wa Usajili Mpya na Rekodi Mpya
Mbali na kutinga hatua ya fainali ya Ngao ya Jamii, Ahmed Ally alibainisha kuwa matokeo hayo yanaonyesha ubora wa usajili uliofanywa na klabu hiyo katika madirisha yote mawili ya usajili (dirisha kubwa na dogo).
Alitolea mfano mshambuliaji mpya, Mary, aliyesajiliwa hivi karibuni kutoka Fountain Gate katika dirisha dogo, kwamba ameonyesha mchango wa papo hapo kwenye kikosi hicho.
“Ni jambo bora kuona kwamba timu tuliyoiandaa kwa muda mrefu na wachezaji tuliosajili wamekuwa na mchango wa moja kwa moja. Mtazame mchezaji kama Mary, amekuja dirisha dogo kutoka Fountain Gate lakini tayari anaonyesha ni mchezaji aliyekamilika na msaada mkubwa,” alihitimisha Ahmed Ally.