Faisal Richard Mganga Afunguka Sababu ya Kujiunga na IAA SC ya Arusha
BEKI wa kati, Faisal Richard Mganga, ameeleza sababu zilizomfanya achague kujiunga na kikosi cha IAA SC ya Arusha ili kutafuta changamoto mpya katika maisha yake ya soka, kufuatia kumalizika kwa mkataba wake na KenGold FC ya Mbeya mwishoni mwa msimu wa 2025-2026.
Akizungumza kuhusu usajili huo, Faisal alisema kabla ya msimu uliopita kufikia tamati, ilikuwa vigumu kutabiri hatima yake. Lipopatikana ofa kutoka IAA SC, haikumchukua muda mrefu kufanya maamuzi ya kuelekea jijini Arusha.
“Nafasi niliyoipata ni muhimu sana kwangu kuendelea kuonyesha ubora wangu. Nimesaini mkataba wa mwaka mmoja nikiamini kwa ushirikiano wa wachezaji, viongozi na benchi la ufundi, tutaisaidia IAA SC kufanya vizuri licha ya ugeni wetu katika Ligi ya Championship,” alisema Faisal.
Beki huyo mwenye uzoefu mkubwa—ambaye amewahi kuzichezea timu za Mbeya Kwanza, Ruvu Shooting, Namungo FC, Pamba Jiji, Ndanda FC, Tabora United (ambayo sasa ni TRA United), KenGold FC pamoja na Mbeya City—ameongeza kuwa ubora wa wachezaji wapya waliosajiliwa unampa matumaini makubwa ya kufanya vyema msimu huu.
Timu ya IAA SC ya jijini Arusha ilifanikiwa kufuzu kucheza Ligi ya Championship kwa msimu wa 2026-2027 kupitia mechi za ‘Play-Off’, ambapo iliing’oa African Sports ya Tanga kwa jumla ya mabao 3-2 (ikishinda 2-1 nyumbani na kutoka sare ya 1-1 ugenini).