Hussein Rupia KenGold FC
Michezo

KenGold FC Yampa Mkataba Hussein Rupia Kurejesha Heshima Mbeya

Vardo October 4, 2026 6:32 pm

Mabosi wa KenGold FC wamefikia makubaliano ya kumpa mkataba kocha wa zamani wa Stand United ‘Chama la Wana’, Hussein Rupia, ili kuifundisha timu hiyo kwa ajili ya mikikimikiki ya Ligi ya Championship.

Rupia anachukua mikoba ya Jumanne Challe, ambaye ameondoka klabuni hapo na kujiunga na Polisi Tanzania, ambako anakwenda kuwa msaidizi wa kocha Mbwana Makata.

Kocha huyo mpya, ambaye pia ana uzoefu wa kuifundisha Hausung FC ya Njombe, anatua katika kikosi hicho cha jijini Mbeya akiwa na kibarua kizito cha kuhakikisha anakirejesha Ligi Kuu Bara baada ya kushuka daraja.

Akizungumzia changamoto hiyo mpya, Rupia amebainisha kuwa ingawa ni mgeni ndani ya KenGold FC, hana ugeni wowote na ushindani wa Ligi ya Championship na yuko tayari kupambana.

“Ni ugeni wa timu ya KenGold FC lakini sio katika Ligi ya Championship. Nina uzoefu wa kutosha na sasa ni muda wa kuonyesha uwezo wangu hapa. Msimu huu ni mgumu, hivyo lazima tuungane pamoja mimi, viongozi na mashabiki ili kutimiza malengo ya kurejesha heshima ya Mbeya,” alisema Rupia.

Rupia ana rekodi nzuri kwenye ligi za chini, ambapo aliipandisha Hausung FC kucheza Championship baada ya kuongoza Ligi Daraja la Kwanza (Kundi A) kwa pointi 25.

Mashabiki wa KenGold FC sasa wanasubiri kwa hamu kuona kama uzoefu wa Rupia utaisaidia timu hiyo kurejea kwa kasi kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.

Faisal Richard Mganga Afunguka Sababu ya Kujiunga na IAA SC ya Arusha Ballon d’Or 2026: Kwa Nini Mastaa wa EPL Wamekosa Orodha ya Dhahabu?