Ahmed Bakari Pipino
Michezo Bongo

Pipino Ametaja Siri ya Mabadiliko Yake SBS, Amwagia Sifa Jonas Mkude

Vardo October 4, 2026 10:04 am

Nahodha msaidizi wa Singida Black Stars (SBS), Ahmed Bakari Pipino, amebainisha kuwa ushindani mkubwa uliopo ndani ya kikosi hicho umeendelea kumpandisha kiwango na kumfanya kuwa mchezaji bora zaidi uwanjani.

Akizungumzia mwenendo wake msimu huu, Pipino—ambaye tayari anamiliki bao moja—alisema uwepo wa wachezaji wa kigeni wenye ubora pamoja na wazawa wenye uzoefu mkubwa umemsaidia sana kujifunza vitu vipya kila siku.

“Nimeanza msimu vizuri na natarajia utakuwa wenye manufaa makubwa kwangu. Baada ya kujiunga na Singida Black Stars, najiona nina utofauti mkubwa kutokana na vitu vingi ninavyojifunza kutoka kwa wenzangu,” alisema Pipino.

Kiungo huyo wa zamani wa KMC, ambaye kabla ya kutua SBS aliwaniwa kwa kasi na klabu za Simba SC, Yanga SC na Azam FC, aliongeza kuwa ushiriki wa timu hiyo katika michuano ya kimataifa unampa fursa ya kujiandaa na ndoto zake za kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.

Amwagia Sifa Jonas Mkude na Himid Mao

Wakati zamani akimjadili aliyekuwa kiungo wa Yanga na SBS, Khalid Aucho, kama mfano wake wa kuigwa, kwa sasa Pipino amewataja viungo wakongwe Jonas Mkude (Mashujaa FC) na Himid Mao (Azam FC) kuwa ndio walimu wake wakuu uwanjani.

“Ukiwatazama Mkude na Mao uchezaji wao, kuna kitu kikubwa sana cha kiufundi unajifunza. Hawatumii nguvu nyingi bali wanatumia akili kubwa—wanajua muda sahihi wa kupokonya mpira na wakati sahihi wa kupiga pasi za maamuzi,” alihitimisha Pipino.

Kompyuta Yaonyesha Hatari Ya Adhabu Ya Manchester City Kushuka Daraja