Daddy Francis Afichua Mfumo Unavyoibeba Vibaya Chipukizi ZPL
Kiungo mshambuliaji wa Chipukizi FC, Daddy Francis, ameweka wazi kuwa mfumo wa mchezo unaotumiwa na timu hiyo hivi sasa ndiyo chanzo kikuu cha wao kukosa matokeo chanya kwenye Ligi Kuu ya Zanzibar (ZPL).
Francis ameeleza kuwa Chipukizi inatumia mfumo unaozingatia zaidi kujilinda badala ya kushambulia, jambo linalotoa fursa kwa timu pinzani kufanya mashambulizi ya mfululizo na hatimaye kuwachosha wachezaji.
Akitolea mfano mchezo wao dhidi ya Zimamoto uliochezwa Septemba 30, 2026, amesema walipoteza kwa bao 1-0 kutokana na safu ya ulinzi na golikipa kuchoka kuhimili mikimiki ya wapinzani baada ya kuzidiwa.
“Timu inajilinda sana kuliko kushambulia, ndio maana tunafungwa. Wachezaji wanachoka kuzuia mashambulizi ya timu pinzani hadi tunaruhusu mabao licha ya kupambana kwa jasho na damu,” alisema Daddy Francis.
Kiungo huyo ameongeza kuwa kikosi chao tayari kina muunganiko mzuri na kama ingekuwa inalinda na kushambulia kwa usawa, kusingekuwa na sababu ya kupoteza mechi.
Kutokana na hali hiyo, Francis amemwomba Kocha Mkuu wa Chipukizi, Suleiman Mohamed ‘Mani Gamera’, kufanya mabadiliko ya mbinu na mfumo haraka iwezekanavyo ili kuinusuru timu hiyo isitumbukie kwenye janga zito zaidi.
Chipukizi inajiandaa kushuka dimbani Oktoba 9, 2026, kuwakabili Mwenge kwenye Uwanja wa Gombani uliopo Pemba, mchezo unaotarajiwa kuwa wa vuta-nikuvute kwani timu zote zinahitaji pointi tatu muhimu.
Kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Zanzibar (ZPL), Chipukizi inashika nafasi ya 15 ikifuatiwa kwa karibu na Mwenge iliyo nafasi ya 14, zote zikiwa zimekusanya pointi 4 pekee baada ya kucheza mechi 6.