Nickson Kibanage Simba SC
Simba SC

Kibanage Atoa Onyo Simba SC: “Msibweteke, Mbele Kuna Dabi na Champions League!”

Vardo October 6, 2026 11:03 am

Beki wa kushoto wa Simba SC, Nickson Kibanage, amewataka wachezaji wenzake, benchi la ufundi pamoja na viongozi wa klabu hiyo kuweka pembeni sherehe za matokeo mazuri ya mwanzo wa msimu na badala yake kuongeza umakini mkubwa kwa ajili ya michezo migumu inayowakabili mbele yao.

Kibanage ameeleza kuwa ingawa kiwango kizuri ambacho Simba SC imekionyesha katika michezo ya hivi karibuni kimerudisha furaha na imani kubwa kwa mashabiki, hali hiyo haipaswi kuwa sababu ya wao kuridhika au kubweteka.

“Si rahisi kucheza vizuri na kupata matokeo mazuri mfululizo. Tunawapongeza wachezaji wenzangu, benchi la ufundi na viongozi. Mashabiki wamekuwa na imani kubwa na timu yao, lakini kikubwa sasa ni kutokubweteka. Tunahitaji kuwa na concentration ya hali ya juu na kuangalia malengo makubwa ya klabu yetu,” amesema Kibanage.

Siri ya Mshikamano Ndani ya Kikosi cha Simba SC

Akizungumzia hali ya hewa ndani ya vyumba vya kubadilishia nguo (dressing room), Kibanage amefichua kuwa siri kubwa ya ubora wa Simba msimu huu ni upendo na ushirikiano uliopo miongoni mwa wachezaji wote, hata wale ambao hawapati nafasi ya kucheza mara kwa mara.

“Unaona kabisa kuna upendo mkubwa kati ya wachezaji na uongozi wetu. Hata mchezaji ambaye hapati nafasi ya kucheza kwenye mechi anakuwa wa kwanza kumsapoti yule anayecheza. Hiyo ‘spirit’ ndiyo inayoifanya timu iwe imara. Tukiendelea hivi, naamini tutafika mbali sana, si tu kwenye Ligi Kuu bali pia kwenye mashindano ya kimataifa,” aliongeza beki huyo.

Kuelekea Dabi ya Kariakoo na CAF Champions League

Beki huyo alisisitiza kuwa pointi tatu wanazozipata kwenye Ligi Kuu ni hatua nzuri kwenye mbio za ubingwa, lakini mtihani mkubwa upo kwenye michezo ijayo ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF Champions League) pamoja na Dabi ya Kariakoo.

Kibanage amewahakikishia mashabiki wa Msimbazi kuwa wachezaji wote wanatambua uzito wa jezi ya Simba na matarajio makubwa yaliyopo msimu huu, na kwamba wapo tayari kupambana kufikia malengo hayo kupitia nidhamu na umoja.

Yanga Princess Yapata Mrithi wa Edna Lema: Mjerumani Martin Hammel Kuchukua Mikoba? Ahmed Ally: Simba vs Yanga Ndio Kipimo Halisi Cha Ubora Wetu Msimu Huu!