Simba vs Yanga Kariakoo Dabi
Simba SC

Ahmed Ally: Simba vs Yanga Ndio Kipimo Halisi Cha Ubora Wetu Msimu Huu!

Vardo October 6, 2026 11:08 am

DAR ES SALAAM: MENEJA wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, ameweka wazi kuwa mchezo wao wa watani wa jadi (Kariakoo Dabi) dhidi ya Yanga SC utakuwa kipimo halisi cha kuthibitisha ubora wa kikosi chao kwa msimu huu, licha ya kuanza kwa kasi kishindo katika Ligi Kuu Tanzania Bara.

Simba tayari imeingia kwenye kambi ya ndani kuelekea dabi hiyo kufuatia kurejea nchini siku ya Jumatatu kutoka Afrika Kusini, ambako walikuwa wameweka kambi ya siku 10 kujiweka sawa.

Kambi ya Afrika Kusini na Maandalizi ya Mo Simba Arena

Akimzungumzia mchezo huo wa Oktoba 10, Ahmed Ally amethibitisha kuwa kambi yao ya Afrika Kusini ilikuwa na mafanikio makubwa na sasa kikosi kimehamishia maandalizi yake kwenye Uwanja wa Mo Simba Arena.

“Alhamdulillah tumerejea salama kutoka Afrika Kusini ambako tulikuwa na kambi ya siku 10 na kambi yetu imekwenda barabara kweli kweli. Leo tunaanza kambi ya ndani kuelekea mchezo wetu wa Kariakoo Dabi,” amesema Ahmed.

Wachezaji wa Timu za Taifa na Morali ya Kikosi

Ahmed ameongeza kuwa wachezaji wote waliokuwa kwenye majukumu ya timu zao za taifa wanatarajiwa kuungana na wenzao muda wowote. Pia ameweka wazi kuwa morali ndani ya timu ipo juu sana kutokana na ukubwa na uzito wa mchezo huo.

“Morale ni kubwa sana. Wachezaji wameutazama mchezo huu kwa jicho la matamanio makubwa, kiasi kwamba tuliamua kuwapeleka mpaka Nanjii kuweka kambi. Ujumbe ulikuwa kwamba sisi tuko serious kwenye hii mechi ya tarehe 10 na michezo mingine inayofuata,” ameeleza.

Rekodi ya Ushindi na Kipimo cha Dabi

Hadi sasa, Simba imeanza msimu kwa kishindo baada ya kushinda michezo yake yote mitano dhidi ya Kagera Sugar, Pamba Jiji, Singida Black Stars, Coastal Union na Azam FC. Hata hivyo, Ahmed amesisitiza kuwa matokeo hayo bado hayajawapa kiburi.

“Simba na Yanga ni mechi ya kipimo, ni mchezo ambao unakwenda kupata ubora halisi wa timu yako. Tumeshinda mechi tano dhidi ya Azam, Singida, Pamba, Kagera na Coastal Union, lakini hicho hakitoshi kuwa kipimo cha kujiridhisha kwamba tunayo timu bora ya kushindana msimu huu,” aliongeza Ahmed Ally.

Hali ya Hewa na Hali ya Timu

Meneja huyo amehitimisha kwa kusema kuwa hakuna changamoto yoyote inayowakabili kwa sasa, na hata mvua zinazoendelea kunyesha jijini Dar es Salaam hazitavuruga mipango yao ya kuchukua pointi tatu muhimu.

Kibanage Atoa Onyo Simba SC: “Msibweteke, Mbele Kuna Dabi na Champions League!” Nickson Kibabage Apona Majeraha Simba SC, Agusia Dabi ya Kariakoo!