Nickson Kibabage Simba SC
Simba SC

Nickson Kibabage Apona Majeraha Simba SC, Agusia Dabi ya Kariakoo!

Vardo October 6, 2026 11:20 am

BEKI wa kushoto wa Simba SC, Nickson Kibabage, amewatoa hofu mashabiki wa klabu hiyo baada ya kutangaza kuwa anaendelea kurejea taratibu katika hali yake ya kawaida kufuatia kukaa nje ya uwanja kwa takribani mwezi mmoja kutokana na majeraha.

Kibabage alipata majeraha hayo katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Pamba Jiji FC. Hata hivyo, amethibitisha kuanza mazoezi mepesi baada ya kupata ruhusa rasmi kutoka kwa madaktari wa timu hiyo.

“Nilikaa nje mwezi mmoja na nimerudi katika hali nzuri. Kwa sasa nina wiki ya kuanza mazoezi kidogo kidogo na ninaamini nitakuwa vizuri kwa mujibu wa madaktari. Nitakuwa bora huko mbeleni na ninaamini nitarudia katika hali yangu ya kawaida,” alisema Kibabage.

Ushindani wa Namba na Ushirikiano na Mlingo

Akizungumzia ushindani wa namba ndani ya kikosi cha Wekundu wa Msimbazi, Kibabage alieleza kuwa changamoto hiyo ni nguzo muhimu ya kusaidia wachezaji kukuza viwango vyao uwanjani.

Aliongeza kuwa ushindani katika nafasi ya beki wa kushoto unampa kocha Steve Barker wigo mpana wa uchaguzi, huku akibainisha ushirikiano mzuri uliopo kati yake na mchezaji mwenzake, Mlingo.

“Ushindani wa namba unamfanya mchezaji akue kwa kiwango. Kama mchezaji unataka kukua, lazima upende changamoto na unayeshindania namba awe na ubora mzuri. Ukiangalia mimi kama sipo na Mlingo akiwepo, unaona kabisa hakuna tofauti kikosini kwani tunarekebishana na kusaidiana sana,” alifafanua.

Vipi Kuhusu Dabi ya Kariakoo Dhidi ya Yanga?

Kuelekea pambano linalosubiriwa kwa hamu la Dabi ya Kariakoo dhidi ya Yanga SC linalotarajiwa kupigwa Oktoba 10, Kibabage alibainisha kuwa hawezi kuthibitisha moja kwa moja kama atakuwepo uwanjani.

Alieleza kuwa uamuzi wa mwisho wa yeye kucheza upo chini ya Kocha Mkuu na benchi la ufundi, kulingana na utimamu wake wa mwili kwani amerejea mazoezini hivi karibuni.

Ahmed Ally: Simba vs Yanga Ndio Kipimo Halisi Cha Ubora Wetu Msimu Huu! Kimoto Aingiza Falsafa Mpya Singida Black Stars | Ligi Kuu NBC