Kombe la EPL Kuwasili Tanzania Kesho: Kila Kitakachojiri Dar es Salaam!
DAR ES SALAAM, TANZANIA — TUKIO la kihistoria linatarajiwa kutokea nchini kesho Ijumaa, Oktoba 9, wakati Kombe rasmi la Ligi Kuu England (EPL) litakapowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam, likiambatana na viongozi wa juu wa ligi hiyo maarufu duniani.
Tukio hili adhimu linalenga kuwapa mashabiki wa soka nchini Tanzania fursa ya kipekee na ya nadra ya kuliona kombe hilo kwa karibu na kupiga nalo picha.
Ratiba na Muda wa Kuwasili Kombe la EPL
Akizungumza katika hafla ya kutambulisha ujio huo, Mkuu wa Uvumbuzi wa Masoko wa Serengeti Breweries Limited (SBL), Henry Esihaba, amethibitisha kuwa ndoo hiyo maarufu duniani itatua saa 3:00 asubuhi katika Uwanja wa Ndege wa JNIA.
Ujio huu umezeshwa kwa ushirikiano wa Guinness—mdhamini mkuu wa upande wa vinywaji wa EPL—pamoja na SBL, ikiwa ni mara ya kwanza kabisa kwa Kombe la EPL kuletwa nchini Tanzania.
“Ni fursa ya mara moja katika maisha ambayo haijawahi kutokea. Sisi kama Serengeti Breweries Limited tunajivunia kuwa kampuni ya kwanza kuleta Kombe hili pendwa nchini Tanzania,” amesema Esihaba.
Fursa kwa Viongozi na Wadau wa Soka Tanzania
Mbali na mashabiki, ujio wa viongozi wa EPL utatoa fursa kubwa kwa viongozi wa klabu za Ligi Kuu ya NBC pamoja na wadau wa michezo nchini kukutana, kubadilishana uzoefu, na kujifunza mbinu mpya za kuendeleza mpira wa miguu.
Pia, viongozi hao kutoka Uingereza watapata nafasi ya kushuhudia moja kwa moja mapenzi makubwa na hamasa waliyo nayo Watanzania katika mchezo wa mpira wa miguu.
Burudani na Shughuli Mbalimbali
Guinness na SBL zimeandaa matukio na burudani mbalimbali zitakazowakutanisha mashabiki wa soka kuanzia kesho Ijumaa hadi Jumamosi, Oktoba 10, ili kuongeza msisimko na furaha kwa wadau wote wa mchezo huo.
