Kombe la Ligi Kuu England (EPL) Kutua Tanzania: Ratiba na Maeneo Litakapopita Dar
AFISA Michezo Mwandamizi kutoka Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Charles Maguzu, amesema ujio wa Kombe la Ligi Kuu England (EPL) nchini Tanzania utakuwa chachu kubwa ya kuhamasisha maendeleo ya soka na kukuza ushirikiano wa kimataifa katika michezo.
Maguzu amesema ujio wa kombe hilo utawapa Watanzania fursa ya kuliona kwa macho kombe ambalo kwa muda mrefu wamekuwa wakilifuatilia kupitia televisheni, huku akiamini tukio hilo litaongeza hamasa kwa wadau wa soka nchini.
“Katika soka la Tanzania, tunaamini kabisa ujio wa kombe hili utakuwa ni hamasa na chachu kubwa kwa wadau wa soka Tanzania. Kikombe ambacho tunapenda kukishabikia tukiwa kwenye screen nchini Tanzania, kikiwa kinagombewa kwenye Ligi Kuu ya Uingereza, sasa kinawasili hapa nchini tutakiona live,” amesema Maguzu.
Amesema tukio hilo pia linaweza kufungua milango ya ushirikiano zaidi kati ya sekta binafsi, mashirika ya ndani na nje ya nchi pamoja na Serikali, katika kuendeleza na kuitangaza michezo ya Tanzania kwenye jukwaa la kimataifa.
Maguzu amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kesho, Oktoba 9, katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kuanzia saa tatu asubuhi kulipokea kombe hilo, kabla ya kuzungushwa katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam kwa mujibu wa ratiba.
Aidha, amewataka mashabiki kujitokeza Oktoba 10 kwenye Uwanja wa KMC, ambako pamoja na shughuli mbalimbali za kombe hilo, watapata nafasi ya kutazama Dabi ya Kariakoo kati ya Simba na Yanga inayotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Uhuru.

“Tunafahamu Watanzania watakaokuwa na hamu ya kuangalia derby ni wengi na capacity ya Uwanja wa Uhuru si kubwa kubeba wote. KMC wamejitolea kuwepo na wataweka screen kubwa ili mashabiki waweze kuangalia mchezo huo,” amesema.
Kwa upande mwingine, Maguzu amesema ujio wa kombe hilo unaendana na juhudi za Tanzania kuimarisha miundombinu ya michezo kuelekea AFCON 2027, akitaja ujenzi na ukarabati wa viwanja mbalimbali nchini.
Amesema Tanzania imeendelea na ujenzi wa viwanja vya kisasa Arusha na Zanzibar, huku Uwanja wa Benjamin Mkapa na Uwanja wa Uhuru ukiendelea kufanyiwa maboresho pamoja na viwanja vya mazoezi.
Maguzu pia amewataka vijana kutumia ujio wa kombe hilo kama hamasa ya kuendeleza vipaji vyao, akisisitiza kuwa soka linaweza kuwa chanzo cha ajira na mafanikio endapo wataweka bidii katika mazoezi na kusikiliza maelekezo ya makocha.
“Tutumie fursa hii kwa vijana kuibua vipaji, kuongeza bidii ya mazoezi na kusikiliza walimu kwa umakini ili wakuze vipaji vyao na kupata fursa ya kwenda kucheza kwenye Ligi Kuu ya Uingereza. Ndoto za kupata fedha za kigeni kupitia mpira wa miguu ziweze kutimia,” amesema.
Maguzu amewapongeza pia waandishi wa habari kwa kushiriki katika tukio hilo, akiwataka kuendelea kuhamasisha umma kuhusu ujio wa kombe hilo na umuhimu wake kwa soka la Tanzania.
“Inabidi muone kwa macho yenu jinsi mapenzi ya soka yalivyo hapa Tanzania. Hii ndiyo maana kombe limekuja hapa. Hakuna mahali pengine Afrika ambapo upendo wa soka uko kama hapa,” amesema.