Kombe la Ligi Kuu ya Uingereza Lawasili Tanzania kwa Mara ya Kwanza!
Dar es Salaam, Tanzania: Kombe halisi la Ligi Kuu ya Uingereza (English Premier League) limetua rasmi nchini Tanzania kwa mara ya kwanza kabisa katika historia, likiashiria mwanzo wa ziara yake kubwa ya Afrika Mashariki.
Tukio hili la aina yake limefanikishwa na chapa ya bia ya Guinness, ambao ni wadhamini rasmi wa vinywaji wa Ligi Kuu hiyo inayopendwa zaidi duniani. Kuwasili kwa kombe hili kunafungua pazia la sherehe za siku mbili zitakazounganisha hadhi ya EPL na utamaduni wa kipekee wa soka la Mtanzania.
Guinness Waleta Ladha ya Soka la Kimataifa Nchini
Kwa Guinness na kampuni mama ya Serengeti Breweries Limited (SBL), kuleta kombe hili si tu kuonyesha alama hii kubwa ya mchezo wa mpira wa miguu, bali ni kutengeneza fursa inayounganisha soka la kimataifa na nguvu, ubunifu, pamoja na mapenzi ya dhati ya Watanzania kwa mchezo huu.
Akizungumza kuhusu ujio huo wa kihistoria, Mkurugenzi Mtendaji wa Serengeti Breweries, Dk. Obinna Anyalebechi, alisema:
“Ligi Kuu ya Uingereza ina nafasi kubwa sana katika mioyo na mazungumzo ya kila siku ya mamilioni ya Watanzania. Kinachofanya tukio hili kuwa cha kipekee ni kwamba sasa Kombe lenyewe limefika hapa, likikutana na mashabiki mahali ambapo mapenzi yao kwa soka yanaishi. Tunataka kuandaa tukio lenye ladha halisi ya Kitanzania na kuipa dunia fursa ya kuona hamasa yetu.”
Mashabiki wa Simba na Yanga Waungana Kwenye Hamasa
Ujio wa Kombe la EPL umeingia moja kwa moja kwenye mishipa ya utamaduni wa soka nchini. Mashabiki wa miamba ya soka Tanzania, Simba SC na Young Africans (Yanga SC), wamekuwa sehemu kubwa ya hamasa hiyo, kwani wengi wao pia ni wafuasi wakubwa wa vilabu vya Uingereza.
Mkurugenzi wa Masoko na Ubunifu wa Serengeti Breweries, Henry Esiaba, aliongeza kuwa:
“Tanzania ina utamaduni mkubwa na wa pekee wa soka. Katika safari hii ya Afrika Mashariki, tunataka Kombe hili liwe sehemu ya simulizi na sherehe zitakazoongozwa na mashabiki wenyewe wa Kitanzania.”
Viongozi wa Soka na Serikali Wanena
Mwakilishi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Aaron Nyanda, alibainisha kuwa kuwasili kwa kombe hilo kunaonyesha uhusiano wa karibu uliopo kati ya soka la ndani na lile la kimataifa:
“Tukio hili linathibitisha jinsi mashabiki wa Tanzania wanavyofuatilia soka la ngazi zote na linawapa fursa ya kipekee ya kukutana na alama hii kuu ya soka duniani.”
Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Makonda, aliyehudhuria mapokezi hayo, alisisitiza umuhimu wa michezo katika jamii:
“Michezo huwaleta watu pamoja na kutengeneza fursa kwa vijana. Kuwasili kwa Kombe la Ligi Kuu ya Uingereza ni fursa nyingine ya kuonyesha nafasi kubwa ambayo michezo inachukua katika taifa letu.”
Ratiiba ya Kombe kuendelea Afrika Mashariki
Baada ya kukamilisha sherehe na matukio mbalimbali jijini Dar es Salaam, Kombe la Premier League litaendelea na ziara yake nchini Uganda kuanzia tarehe 11 hadi 13 Oktoba, kabla ya kuhitimisha safari yake nchini Kenya.