Dabi ya Kariakoo Simba vs Yanga
Simba SC

Dabi ya Kariakoo: Simba Yatangaza Viingilio na Hali ya Kikosi Dhidi ya Yanga

Vardo October 8, 2026 12:36 pm

Klabu ya Simba SC imeweka wazi kuwa maandalizi yake kuelekea mchezo wa Dabi ya Kariakoo dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga SC, yanaendelea vizuri huku ikitangaza rasmi viingilio vya pambano hilo linalosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka nchini.

Mchezo huo wa kukata na shoka unatarajiwa kupigwa Jumamosi, Oktoba 10, kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Maandalizi ya Kikosi Chini ya Steve Barker

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, ameeleza kuwa maandalizi ya mchezo huo yalianza mapema kule nchini Afrika Kusini, ambako Kocha Mkuu Steve Barker alikuwa na kambi ya siku 10.

Akiwa huko, Kocha Barker alitumia michezo miwili ya kirafiki kukisuka na kukinoa kikosi hicho vizuri kabla ya kurejea jijini Dar es Salaam Oktoba 4.

“Maandalizi yanaendelea vizuri sana. Kocha Steve Barker alianza maandalizi hayo kwenye kambi pale Afrika Kusini, ambako amekuwa na siku 10 bora sana pamoja na mechi mbili nzuri za kirafiki,” amesema Ahmed Ally.

Ahmed ameongeza kuwa kikosi kimeingia kambini rasmi nyumbani kujiandaa na pambano hilo:

“Baada ya hapo, Oktoba 4 tukarejea Dar es Salaam na juzi tukaingia rasmi tena kambini kwa ajili ya kuanza maandalizi tukiwa hapa nyumbani kuelekea kwenye mchezo wa Oktoba 10.”

Hali ya Wachezaji Kambini

Nyota wengi wa Simba tayari wamewasili kambini na kuungana na wenzao. Wachezaji waliokuwa kwenye majukumu ya timu ya taifa (Taifa Stars) walianza kurejea na kuingia kambini mara moja.

Hata hivyo, wachezaji wawili pekee, Inno Loemba na Mahmadou Sillah, ndio waliokuwa bado wanakamilisha majukumu ya timu zao za taifa kabla ya kujiunga na kikosi.

Viingilio vya Dabi ya Kariakoo (Simba vs Yanga)

Upande wa maandalizi ya kiutawala, Simba imethibitisha kuwa kila kitu kimekamilika na kutangaza rasmi viingilio vya mchezo huo utakaofanyika Uwanja wa Uhuru.

Viingilio vimepangwa kama ifuatavyo:

  • VIP: Tsh 50,000

  • Mzunguko: Tsh 20,000

Ahmed Ally amebainisha kuwa Uwanja wa Uhuru una majukwaa ya aina mbili tu (VIP na Mzunguko), hivyo mashabiki wametakiwa kukata tiketi zao mapema ili kuepuka usumbufu siku ya mchezo.

Kombe la Ligi Kuu ya Uingereza Lawasili Tanzania kwa Mara ya Kwanza! Siri Yafichuka: Namna Simba SC Ilivyomnusuru Ibrahim Doumbia Kwenye Presha Msimbazi