Mangungu Afunguka: Yanga Walipaswa Kufungwa Mabao Mengi Zaidi!
Mwenyekiti wa Simba SC, Murtaza Mangungu, amewatambia watani zao wa jadi, Yanga, akisisitiza kuwa ushindi wao mtamu wa mabao 2-1 katika Dabi ya Kariakoo haukuwa wa kubahatisha, bali ni dhihirisho la ubora wa kikosi chao huku akidai wapinzani hao walinusurika kupata kipigo kikubwa zaidi.
Simba iliibuka na ushindi huo muhimu katika pambano lililopigwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, matokeo yaliyowasha shangwe kubwa kwa mashabiki na wanachama wa Mnyama. Akizungumzia mchezo huo uliokuwa na ushindani mkubwa, Mangungu alieleza kuridhishwa kwake na namna wachezaji walivyojituma uwanjani.
Licha ya kukiri kuwa kulikuwa na makosa madogo yaliyowapa Yanga bao, kiongozi huyo alieleza kuwa kikosi chake hakikupoteza mwelekeo wala kuyumba kisaikolojia.
“Wale ambao wamekaa kimya walie, ambao walikuwa wanalia walie, na ambao walikuwa wanacheka waendelee kufanya hivyo. Hilo ni juu yao. Sisi tunaangalia mambo yetu, tumeandaa timu ambayo imekuja na kufanya vizuri leo,” alisisitiza Mangungu.
Simba Ilikuwa na Uwezo wa Kushinda Sana
Mangungu alikwenda mbali zaidi na kuweka wazi kuwa Yanga ilikuwa na bahati ya kuondoka na kipigo kidogo, akidai kuwa kama si kukosa umakini na mpira kugonga mwamba mara mbili, Simba ingeweza kuibuka na ushindi wa zaidi ya mabao matatu.
“Siyo tu kwamba tumewafunga, tumewafundisha mpira. Ukiangalia, kama tungekuwa na bahati na umakini zaidi, wangeweza kufungwa zaidi ya mabao matatu. Mipira miwili imegonga mwamba, achana na nafasi nyingine,” aliongeza.
Ushindi huo wa 2-1 unampa jeuri kubwa uongozi wa Simba huku ukithibitisha utayari wa kikosi hicho kukabili presha ya mechi kubwa na kuendelea kusaka mafanikio katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.