Ndoto Yetu ni Ubingwa wa Afrika – Mo Dewji Aweka Wazi Malengo ya Simba
Rais na mwekezaji wa klabu ya Simba SC, Mohammed Dewji ‘Mo’, ameweka wazi kuwa kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya sita ni hatua kubwa na ya kujivunia, lakini haitoshi kwani ndoto kuu ya klabu hiyo ni kutwaa taji la ubingwa wa Afrika.
Akizungumzia mafanikio hayo, Mo Dewji amewapongeza wachezaji, benchi la ufundi, viongozi, na mashabiki wote kwa mchango wao mkubwa uliowezesha Simba kufika hatua hiyo ya makundi kwa mara ya sita katika historia ya klabu. Alisema mafanikio haya yanatokana na uwekezaji wa muda mrefu, mipango madhubuti, pamoja na nidhamu ya hali ya juu.
“Hongera kwa wachezaji, benchi la ufundi, viongozi na mashabiki wote wa Simba SC kwa kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Mara sita kufuzu si jambo dogo; ni matokeo ya miaka ya uwekezaji na dhamira ya kujenga Simba yenye ushindani mkubwa barani Afrika,” alisema Mo Dewji.
Hata hivyo, bilionea huyo alisisitiza kuwa Simba haijaridhika na hatua ya makundi pekee, bali inalenga kupambana ili kuandika historia mpya barani Afrika kwa kutwaa ubingwa huo mkubwa.
“Tumetoka mbali, lakini malengo yetu ni makubwa zaidi. Tunajivunia hatua tulizopiga, lakini hatujaridhika. Ndoto yetu ni kutwaa ubingwa wa Afrika. Safari inaendelea,” alihitimisha.
Kauli hii inazidi kuchocheahamasa na kuweka wazi matarajio makubwa ya Wekundu wa Msimbazi msimu huu katika michuano ya kimataifa.