Simba SC Yazungumza Hili Baada ya Kutinga Makundi Ligi ya Mabingwa Afrika
KOCHA Mkuu wa Simba SC, Steve Barker, amewasha moto na kutangaza wazi kuwa malengo ya timu hiyo sasa ni kufika hatua ya mtoano (Robo Fainali na kuendelea) baada ya kukamilisha lengo la kwanza la kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.
Simba imefuzu kwa kishindo baada ya kuwanyuka 15 de Agosto ya Equatorial Guinea mabao 3-0 katika mchezo wa marudiano uliopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, na kufuzu kwa jumla ya mabao 9-1 kufuatia ushindi wa 6-1 ugenini.
Akizungumza mara baada ya mchezo huo kumalizika, Kocha Barker alionyesha kufurahishwa na kiwango cha wachezaji wake na kusisitiza kuwa kikosi hicho kimejipanga kufanya makubwa zaidi katika hatua inayofuata.
“Lengo letu la kwanza lilikuwa ni kufuzu hatua ya makundi. Sasa tumetimiza hilo na tunasubiri droo ya wiki hii. Tukifika huko, lengo letu kuu ni kufuzu hatua ya mtoano,” alisema Barker kwa kujiamini.
Kikosi Kiko Tayari kwa Ushindani
Akizungumzia mabadiliko yaliyofanyika katika kikosi kilichoanza mchezo huo wa marudiano, Barker alieleza kuwa yalilenga kuwapa mapumziko baadhi ya nyota huku akiwapa nafasi wachezaji wengine kuonyesha uwezo wao kabla ya kurejea kwenye michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Pamoja na ushindi huo mnono wa jumla, kocha huyo alibainisha kuwa benchi la ufundi litafanya tathmini ya kina ili kurekebisha makosa madogo madogo yaliyojitokeza, akitambua kuwa ushindani utakuwa mkubwa zaidi katika hatua ya makundi.
“Kushinda mabao 9-1 ni jambo kubwa sana kwetu. Tunajivunia kiwango kilichoonyeshwa na wachezaji mmoja mmoja na timu kwa ujumla. Sasa tunasubiri kupata wapinzani wetu kwenye droo ili tuanze maandalizi maalum ya kila mchezo mmoja baada ya mwingine,” aliongeza.