De Reuck: Simba Bado Ina Nafasi Kubwa ya Kufanya Vizuri Afrika
BEKI mahiri wa Simba SC, Rushine De Reuck, ameweka wazi kuwa pamoja na timu hiyo kuendelea kutamba katika mashindano ya kimataifa, bado ina nafasi kubwa ya kuboresha kiwango chake ili kufikia malengo iliyojiwekea ya kutwaa ubingwa na kufanya vizuri zaidi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
De Reuck aliyasema haya kufuatia ushindi wa jumla wa Simba SC kwenye mchezo wa marudiano wa raundi ya pili ya awali dhidi ya 15 de Agosto, uliopigwa Oktoba 25, 2026, katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Beki huyo raia wa Afrika Kusini alieleza kufurahishwa kwake kuwa sehemu ya kikosi hicho kinachoonyesha kiwango cha juu, akisema kuwa ushindani wa namba, mshikamano, na moyo wa kujituma ndio siri kubwa ya mafanikio yao.
Kuhusu mabadiliko yaliyofanywa na Kocha Mkuu, Steve Barker, De Reuck alipongeza jinsi wachezaji wote walivyotumia vizuri nafasi zao kuonyesha uwezo wao, jambo linaloashiria upana na ubora wa kikosi hicho kwa msimu huu.
“Lengo letu ni kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Tulifanya mabadiliko mengi, lakini kila mchezaji aliyepewa nafasi alionyesha uwezo mkubwa. Hilo linaonyesha mshikamano tulionao,” alisema De Reuck.
Aidha, beki huyo alisisitiza kuwa badala ya kuanza kuwaza wapinzani wao, wanapaswa kujikita zaidi katika kujitathmini na kuendelea kujenga timu imara zaidi.
“Ni muhimu kwetu kuangalia tunachokifanya na kuendelea kuboresha. Tunafanya vizuri kwa sasa, lakini bado tuna nafasi ya kuimarika zaidi. Tunataka kuendelea kukua kama timu,” aliongeza.